Kutokana na malalamiko ya mara kwa mara kwa wananchi kuhusu kukosa huduma ya runinga za bure pindi vifurushi katika visimbusi (ving’amuzi) vyao vinapomalizika, serikali imetolea ufafanuzi suala hilo kwa kueleza namna mfumo wa utendaji unavyotakiwa kufanya kazi.
Akijibu maswali ya watumiaji mbalimbali wa mtandao wa Twitter kuhusu urushwaji wa runinga za bure, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Abbas alisema, kwa mujibu wa sheria iliyopo sasa, vituo vyote vya runinga ambavyo vimepewa leseni ya FTA (Free to Air) vinapaswa kuonekana hata baada ya kifurushi kwenye kisimbusi kwisha.
Dkt. Abbas alisema kwamba, hadi sasa kuna vituo 16 vya runinga vya ndani ya nchi vilivyopewa leseni hizo, vikiwemo vituo vya ITV, Clouds TV na Channel 10.
Aidha, alifafanua kuwa, ili mtumiaji aweze kutazama hata baada ya kufurushi chake cha malipo kwisha, kituo cha runinga (mfano ITV) kinapaswa kuwalipa warushaji wa masafa (mfano Azam) ili ITV iweze kuonekana kwa wananchi hata ambao hawajalipia visimbusi vyao.
“… mfumo uko hivi: ili wewe uone bure hizo channeli kuna mzalishaji wa vipindi ambaye ni kituo cha TV na msafirisha masafa mfano StarMedia. Ili wewe uone bure kuna gharama huyo wa kwanza anatakiwa kulipia kwa wa pili. Asipolipia akakatiwa huduma hautaona. Kwa sasa ndio mfumo.”
Pia, Dkt. Abbas alitahadharisha kuwa, endapo kituo cha runinga hakutawalipa wasafirishaji wa masafa, watakatiwa huduma na hivyo kuwafanya wananchi washindwe kuweza kutazama runinga bure.
Kuhusu TBC kuonekana katika visimbusi vyote hata bila malipo, msemaji alifafanua kuwa, kila kisimbusi kinatakiwa kuweka TBC kupitia sera ya ‘must carry’ ambayo inaiwezesha kuonekana kwa wananchi bila malipo yoyote.
“Unapata TBC mda wote kwa sababu TBC anahadhi inayoitwa “must carry” ambaye mrusha masafa yeyote Tz lazima aioneshe TBC. Kama hupati channeli zingine za FTA muulize mtoa huduma wako. Majibu atakayokupa nijulishe na unipe jina la mtoa huduma wako,” aliandika Dkt. Abbas.
Alisema kuwa, kwa sasa serikali haina mfumo wa kuwaadhibu wamiliki wa vituo vya runinga wenye leseni za FTA lakini hawawalipi warusha masafa ili wananchi waweze kuona runinga hizo bure, badala yake, warusha matangazo hayo wanatawakati huduma kama hawajalipwa.
“…kwa kanuni iliyoanza Machi mwaka huu, mtoa huduma za TV asipolipa kwa msafirisha masafa anaweza kukatiwa huduma.”
Kuhusu Dstv na Azam kukata matangazo ya runinga za ndani baada ya kifurushi kwisha, Dkt Abbas alisema suala hilo lipo Baraza la Ushindani hivyo wananchi wasubirie majibu, na kwamba asingependa kulizungumzia kwa sasa.