Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaelekea kulikubali ombi la kundi la waumini wa Kiislamu wanaotaka dodoso la dini liingizwe kwenye Sensa ya Watu na Makazi iliyopangwa kufanyika Agosti 26, mwaka huu.
Uamuzi huo ambao umeshawahi kupingwa na Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa, unatajwa kwamba huenda ukatangazwa hivi karibuni baada ya ngazi ya juu ya uongozi “kutafakari” na kubaini kuwa dodoso hilo haliwezi kuathiri umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Vyanzo vya habari vimeihakikishia JAMHURI kuwa msimamo wa Serikali kuhusu suala hilo lililozua mjadala mkali nchini utatangazwa muda si mrefu kuanzia sasa. Imeelezwa kuwa viongozi waandamizi, baada ya kulitafakari jambo hilo, wameona hakuna sababu ya kuliogopa kwa kuwa mataifa mengi duniani yanaweka dodoso la udini kwenye sensa zake. Dk. Chuwa aliwahi kusema kwamba suala la udini na kabila la mtu, si mambo ya kuulizwa kwa sababu maendeleo ya nchi hayapangwi kwa kuzingatia vipengele hivyo.
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, ameshasema msimamo wa taasisi hizo kupinga sensa uko pale pale hadi hapo madai yao, likiwamo la dodoso la ukabila, yatakapokubaliwa. Ponda anampinga Sheikh Mkuu wa Tanzania, Issa bin Shaaban Simba, akisema tangazo lake la kupinga dodoso hilo haliwakilishi Waislamu wote, bali linawakilisha Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Dai la pili la kundi hilo ni kutaka Serikali kushauriana na wawakilishi wa dini, ili iundwe Tume huru ya sensa na iwe na wawakilishi wa dini zote. Dai la tatu la kundi hilo ni la kutaka kipengele cha dini kirejeshwe rasmi katika sensa. Wakati Sheikh Ponda akisema hayo, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imeunga mkono kauli ya Simba.
Akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti wa jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Hamis Mattaka alipinga madai ya kuwekwa kwa dodoso la udini kwenye sensa.
Amesema wao kama jopo la wanazuoni hawaoni tatizo hilo kutokana na umuhimu wake kwa taifa na kuongeza kuwa Sensa ya Watu na Makazi ipo kwa mujibu wa sheria za nchi na imepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake, Ofisa Uhamasishaji Sensa ya Watu na Makazi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Said Amir, alipoulizwa juu ya kukubaliwa kwa dodoso la dini, alisema hana taarifa zozote juu ya suala hilo.
“Hili suala nalisikia kwako, ninachojua ni kwamba kuna makundi yanayotaka suala hilo liingizwe kwenye sensa, lakini hadi sasa hakuna uamuzi wowote uliofikiwa, hilo jambo lipo juu yangu,” alisema.