Na Thompson Mpanji, Mbeya
JESHI la Polisi limesema limefanikiwa kudhibiti matukio ya kiuhalifu yaliyokuwa yanadaiwa kusababishwa na kundi la vijana lililoibuka na kujiita jina la ‘Wakorea Weusi’ ambalo lilionekana kuwa tisho kwa maisha ya wananchi wa mkoa huu na mali zao.
Hivi karibuni mkoani Mbeya kuliibuka hali ya sintofahamu ya hofu kubwa ya maisha ya wakazi wa hapa baada ya kuibuka makundi mbalimbali ya kiuhalifu yakiitwa majina mbalimbali.
Kutokana na hofu hiyo polisi mkoani Mbeya walianzisha msako mkali na kufanikiwa kuwatia mbaroni vijana 42 waliokuwa wanatuhumiwa kwa uhalifu huo. Kiongozi wa kundi hilo lilillokuwa lilokuwa likijiita ‘Wakorea Weusi’ aliyetajwa kwa jina la Kelven Raphael (22), naye amekamatwa. Raphael ni mkazi wa Mwakibete, Bombambili, jijini hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Naibu Kamishna Mohamed Mpinga ameliambia JAMHURI kuwa polisi kwa kushirikiana na wananchi wamefanikiwa kuwakamata vijana hao na kuwaondoa hofu wananchi kuwa waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi.

Kamanda Mpinga amekanusha kundi hilo kuhusika na masuala yeyote ya kisiasa, akasema walikuwa vibaka ambao chanzo na asili ya jina hilo ni vita baridi inayoendelea kusikika katika vyombo mbalimbali vya habari baina ya Korea na Marekani.

“Hawa vijana walianza  kama timu za mpira katika maeneo yao  na hawajatoka nje ya Mkoa wa Mbeya, bali ni vijana wetu tunaoishi nao, na nichukuwe nafasi hii kuwaomba viongozi wa mitaa na wananchi kutoa ushirikiano pindi wanaposikia taarifa zozote  zinazohusiana na uhalifu. Wasisite kuja polisi, ingawa kulikuwa na taarifa kwamba matukio ya uhalifu yalianza kutokea muda mrefu, lakini kumekuwepo na madai ya wananchi kuendelea kunyamaza wakihofia kulipiziwa kisasi pindi [watuhumiwa] wanapofikishwa polisi au mahakamani na kuachiliwa huru na hivyo kuwarudia kuwatisha,” amesema.
  
Ametoa wito kwa  wamiliki wa biashara  za vinywaji kuheshimu sheria za taratibu za muda wa kufunga unapotimia kuepuka wahalifu kutumia mwanya huo kujificha wakasubiri kutekeleza uhalifu. Pia ameiomba jamii kuanzisha mfumo wa ulinzi shirikishi baada ya kupata mafunzo kutoka polisi yenye kuwapa ujuzi jinsi ya kuwabaini na kuwakamata wahalifu.