Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, amepokea transforma kubwa sita katika mradi wa kituo cha kupoza na kupokea umeme cha Chalinze ,zenye uwezo wa megavoti 250 kwa gharama ya Bilioni 7.5 kila moja.

Kuwasili kwa transforma hizo ni muendelezo wa mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 53.13 ,unatarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka huu ambapo hadi kukamilika mradi mzima utagharimu Bilioni 128 fedha kutoka serikalini.

Akipokea transforma hizo,katika kituo hicho huku akiwa ameambatana na ujumbe kutoka Tanesco mkoa , makao makuu na Halmashauri ya Chalinze, Kunenge alisema ,ujio wa kifaa hicho unaandika historia mpya nchini kwani unakwenda kujibu changamoto ya upungufu wa umeme kwenye Maeneo mbalimbali.

Kunenge ameeleza mkoa huo umesheheni kwa viwanda,hivyo hitaji kubwa la wawekezaji ni kupata umeme wa kutosha.

“Tunashukuru Serikali, kwa jitihada za kupunguza tatizo la nishati ya umeme nchini kwa kuendeleza mradi mkubwa wa kimkakati wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere (stigo)litakalozalisha megawatt 2115.”ameeleza Kunenge.

Kwa upande wake meneja miradi Tanesco makao makuu,Didas Lyamuya amefafanua kwamba, shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limeanza kupokea moja ya mashine umba (transforma) sita yenye uwezo wa megavoti 250 katika kituo hicho.

“Kati ya mashine umba hizi sita, mashine umba nne zitakuwa zikipokea umeme mkubwa wa kilovoti 400 utakaosafirishwa kutoka katika mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na kuupoza hadi kilovoti 220 na mashine umba mbili ni kwa ajili ya kuupoza umeme mkubwa kutoka kilovoti 220 hadi kilovoti 132. “

“Mashine umba hizi zina uwezo wa kusafirisha hadi megawati 800 za umeme katika miundombinu ya umeme iliyopo sasa hivi”alieleza Lyamuya.

Hata hivyo Lyamuya alieleza kuwa, kituo hicho kilianza kujengwa mnamo mwaka 2021 na mkandarasi TBEA kutoka China na umefikia asilimia 53.13 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Julai, 2023.

Meneja wa mradi wa kituo Cha kupoza umeme Chalinze, Newton Mwakifwamba alieleza, kukamilika kwa kituo kutasaidia kufupisha njia ya kusafirisha umeme mkubwa kwani sasa umeme mkubwa utakuwa ukisafirishwa kwenda Zuzu Dodoma ili uingizwe kwenye backbone ya Taifa.

“Umeme mkubwa mwingine utasafirishwa kwenda Kinyerezi Dar Es Salaam na mwingine utasafirishwa kwenda Segera Tanga na transforma hii iliyopokelewa moja ni moja ya mashine umba tano na reactors mbili zilizobakia zinatarajiwa kuwasili katika kituo hiki cha kupokea na kupoza umeme mkubwa cha Chalinze tarehe 3, 7, na 17 ya mwezi Machi 2023″amesema Newton.

Meneja Tanesco mkoa wa Pwani,Mahawa Mkaka amewataka wananchi waendelee kuvumilia tatizo la kukatikakatika kwa umeme kutokana na mabadiliko yanayofanyika kutokana ujenzi wa mradi huo.