Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassa, imeiongezea nguvu Bohari ya Dawa (MSD), na kuchangia kuleta mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato.
Lengo la uwekezaji huo ni kuiwezesha MSD iweze kuzalisha, kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za afya katika vituo vya kutolea huduma vya umma na binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dodoma katika kikao kazi na Wahariri vya vyombo mbalimbali vya habari nchini ambao walipata fursa ya kujionea utendaji kazi wa MSD katika baadhi ya kanda, kutembelea Kiwanda cha Kuzalisha Mipira ya Mikono (gloves).
Kiwanda hicho kipo eneo la Idofi-Makambako, mkoani Njombe, pia walijionea usambazaji dawa na vifaa tiba katika Kanda za Iringa pamoja na Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Tukai amesema mapato ya MSD yameongezeka kutokana na uwekezaji mkubwa, maboresho yanayoendelea kufanywa na serikali.
“Mwaka 2022/2023, mapato ya MSD yalikuwa sh. bilioni 359.6 na mwaka 2023/2024 yameongezeka na kufikia sh. bilioni 510.07 sawa na ongezeko la sh. bilioni 150.43 (sawa na asilimia 42),” amesema Tukai.
Amesema mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali iliipatia MSD sh. bilioni 100 kama mtaji wa kuiwezesha Bohari hiyo kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya.
Pia fedha hizo zimetumika kukabiliana na changamoto za mnyororo wa ugavi, kuisadia MSD kuwa na uwezo wa kuhudumia mahitaji ya vituo kwa wakati.
Fedha hizo zimeiwezesha MSD kutengeneza mikakati iliyoifanya Bohari iweze kununua bidhaa za afya kwa tija na kuimarisha mahusiano na wazabuni mbalimbali.
Katika kutekeleza sera ya viwanda, MSD imefanikiwa kuanzisha Kampuni Tanzu ili kuongeza ufanisi wa usimamizi na uendeshaji shughuli za uzalishaji.
Kampuni hiyo inaitwa “MSD Medipharm Manufacturing Company Limited” ambapo Juni 2024, MSD ilizindua Bodi ya Usimamizi wa kampuni hiyo.
“Jukumu la kampuni hii ni usimamizi wa shughuli za uzalishaji wa bidhaa za afya, itakuwa na uwezo wa kuingia ubia na wawekezaji wengine.
“Kwa sasa kampuni hii itasimamia Kiwanda cha Mipira ya Mikono, Idofi-Njombe, eneo la viwanda la Zegereni- Pwani na Kiwanda cha Barakoa-Dar es Salaam,” alieleza.
Akizungumzia mikakati ya mwaka wa fedha 2024/25, alisema MSD itaboresha upatikanaji wa bidhaa za afya na kuweza kujiendesha kibiashara.
Mikakati mingine ni kuongeza uwezo wa kifedha ambapo kupitia mtaji ambao unatolewa na Serikali, MSD itafanya ununuzi wenye tija kutoka kwa wazalishaji hivyo kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya.
Kupitia Kampuni Tanzu, MSD itaendeleza jitihada za kushirikiana na sekta binafsi kuongeza idadi ya viwanda vya bidhaa za afya nchini hivyo kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.
Mikakati mingine ni kuimarisha upatikanaji bidhaa za afya kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo katika Bima ya Afya ya Taifa, kuweza kutambua wahitaji zaidi wa bidhaa hizo nje ya MSD na kuimarisha kitengo cha ndani cha usimamizi wa utendaji.
Kutekeleza ujenzi wa maghala ya kuhifadhia bidhaa za afya katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Ruvuma, Arusha na Geita, kuongeza ufanisi, uwezo wa kuhifadhi dawa na vifaa tiba kwa kujenga maghala, kuangalia maeneo yatakayopunguza gharama za usambazaji.
Pia kuimarisha mifumo ya TEHAMA inayohusu usimamizi wa maghala na ushiriki kwenye kutengeneza mifumo ya NesT, kupitia mifumo inayohusu gharama za uendeshaji (logistiki) kwa kuongeza usimamizi kupitia Idara Maalum ya uendeshaji.
Tukai aliutaja mkakati mwingine ni kuimarisha mifumo ya Utawala, kufanya maboresho ya muundo ili kuendana na utendaji, kufanya tafiti kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kuboresha uendeshaji taasisi zikiwemo Taasisi za Elimu ya Juu.