NA CLEMENT MAGEMBE

Upungufu wa ujuzi wa shughuli za uzalishaji mali, umetajwa kuwa chanzo cha vijana wengi ‘kuwekeza’ zaidi katika michezo ya kubahatisha ili kujipatia kipato.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Ridhiwani Wema, amesema licha ya vijana wengi kuhitimu masomo kwenye vyuo na taasisi za elimu ya juu, wanakosa sifa ya ujuzi zinazohitajika katika kuajiriwa au kujiajiri.

Akizungumza na JAMHURI, Wema amesema baada ya kuona nguvukazi hiyo (vijana) inapotea kwa kujiingiza katika vitendo vya uhalifu na kupoteza muda mwingi bila sababu za msingi, Serikali imeanzisha programu ya kukuza ujuzi kwao.

Wema amesema katika programu hiyo kwa mwaka 2015/2016 hadi 2020/2021 ni utekelezaji wa matokeo ya utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2014 uliobaini, pamoja na mambo mengine, kuwa nchi ina watu 20,030,139 (asilimia 89.7) walioajiriwa katika sekta mbalimbali.

Amesema asilimia 79.9 ya nguvukazi hiyo ilibainika kuwa na kiwango cha chini cha ujuzi wakati asilimia 16.6 walibainika kuwa na kiwango cha kati na asilimia 3.6 walikuwa na kiwango cha juu.

Kutokana na matokeo hayo, ilibainika kuwa upo umuhimu wa Serikali kuhakikisha kuwa nguvukazi iliyo katika soko la ajira inaimarishwa kiujuzi, kufikia viwango vya kimataifa kuwezesha nchi kuwa na uchumi wa kipato cha kati.

Kwa mujibu wa Wema, kiwango cha ujuzi wa nguvukazi unaohitajika ili kukuza uchumi kwa kasi kubwa na kufikia nchi ya kipato cha kati, ni asilimia 12 na kwa nguvukazi yenye kiwango cha juu cha ujuzi ni asilimia 34.

Amesema nguvukazi yenye ujuzi wa kiwango cha kati na isiyozidi asilimia 54 kwa nguvukazi yenye ujuzi wa kiwango cha chini.

Lengo ni kuhakikisha Watanzania wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 45, waliopata stadi za kazi bila kupitia taasisi za mafunzo, wanatambulika kwa kutathmini na kusaini ujuzi walionao na kupewa vyeti vinavyotambulika katika soko la ajira.

Kamari, bahati nasibu

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa idadi ya vijana wanaotegemea michezo ya kubahatisha kwa ajili ya kuwaingizia kipato badala ya kushiriki shughuli za maendeleo, inaongezeka kwenye maeneo tofauti ya nchi.

Mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam, Lucas Mosha, amesema pamoja na tamko la Serikali, jitihada zinazofanywa na mamlaka husika kuwanusuru vijana na ukosefu wa ajira hazionekani katika ngazi za chini kwenye jamii.

Amesema pamoja na michezo ya kubahatisha kuwa sehemu ya burudani, ugumu wa maisha na ukosefu wa mitaji vinachangia vijana kujikita katika michezo ya kubahatisha.

Rajabu Omary, mkazi wa Kunduchi jijini Dar es Salaam na mfanyabiashara wa nguo za mitumba katika soko la Mwenge, amesema michezo ya bahati nasibu inaonekana kama ajira mpya na rahisi kwa washiriki wa mchezo huo.

Naye mfanyakazi wa kampuni ya Supabet iliyoko Mwenge jijini Dar es Salaam, Stella, amelieleza JAMHURI kuwa licha kutoruhusiwa kwa mujibu wa sheria, baadhi ya watu hasa wazazi wamekuwa wakiingia na watoto wadogo kwenye majengo yenye michezo hiyo.

Kwa mtazamo wake, Stella amesema michezo hiyo inakuza ajira kwa wananchi kupitia ajira za wafanyakazi na wanaopata faida kwa kucheza.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini, James Mbalwe, amesema michezo hiyo iko kisheria kwa mujibu wa Sheria namba 4 ya mwaka 2003.

Mbalwe amesema pamoja na mwombaji kutakiwa kutimiza vigezo vinavyotakiwa, lengo linabaki kuwa sehemu ya burudani kwa washiriki na si njia kuu ya kuwaingizia mapato.

Amesema kwa sasa kampuni za michezo ya kubahatisha zilizopo nchini ni 27 ambazo zimesajiliwa kati ya mwaka 2013 hadi mwaka jana.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Richard Kayombo, amesema kampuni zote za michezo ya kubahatisha zinalipa kodi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kayombo amesema hakuna kampuni inayokwepa kulipa kodi kama ilifuata taratibu zote ili kupata usajili na vibali halali vya kuendesha shughuli zake hapa nchini.