Serikali yabisha hodi Epanko

*Wachimbaji wa sasa, wa zamani kikaangoni

*Tume yapelekwa kuchunguza ukwepaji kodi

*Mwekezaji avuna, wananchi waambulia soksi

 

MAHENGE

NA ANGELA KIWIA

Serikali inakusudia kuunda tume ya uchunguzi baada ya kuwapo taarifa za utoroshwaji madini ya spino (spinel) unaofanywa na baadhi ya wachimbaji na wafanyabiasha mkoani Morogoro.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Tanzania, Profesa Shukuru Manya, ameliambia JAMHURI kuwa timu ya uchunguzi itakayoenda Epanko wilayani Ulanga kuchunguza wizi huo, inaundwa wiki hii.

Machi, mwaka huu, JAMHURI lilikuwa gazeti la kwanza kuandika taarifa ya uchunguzi iliyohusu utoroshwaji madini na ukwepaji kodi kwenye madini hayo unaofanywa na wachimbaji na wafanyabiashara wengi.

Katika mahojiano maalumu na JAMHURI yaliyofanyika ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, Profesa Manya amesema Tume na Wizara ya Madini watapeleka wachunguzi Ulanga kupata majawabu ya kukomesha uhujumu unaofanywa na wachimbaji na wafanyabiashara  wanaotuhumiwa.

“Nimesikitishwa na hali ilivyo huko, lakini kwa vile tumetumwa kufanya kazi tutafanya kazi kweli kweli kwani hii fani tunaifahamu na tupo kumsaidia Rais na nchi kwa ujumla…Naibu Waziri (Madini) amejionea hali ilivyo. Naamini ya kuwa wataalamu wetu watabaini mambo mengi zaidi kuliko haya ambayo tumeyaona na kuyasikia,” amesema.

Profesa Manya anasema amebaini kuwapo kwa udhaifu wa usimamizi wa madini na yanauzwa bila kuongezwa thamani.

Ameonyesha kushangazwa na wauzaji kupewa leseni bila kuwa na mashine za kukatia madini; jambo ambalo amesema linahitaji kuchukuliwa hatua za haraka kulikomesha.

“Ninaondoka hapa kichwa kikiwa kinazunguka, natafakari namna ya kutoka hapa. Haiwezekani mtu atoke huko na kuja hapa – ofisi ya wilaya isifahamu, ofisi ya wilaya inatakiwa kuwa na orodha ya leseni zote za uchimbaji madini,” amesema.

Anasema Mahenge ndiko alikoanzia kazi baada ya kuteuliwa na kuthibitishwa na Rais, hivyo atahakikisha sheria na taratibu za uchimbaji na uuzaji madini zinafuatwa kwa mujibu wa sheria.

Ameahidi kufungua ofisi ya madini wilayani Ulanga.

“Spino ni madini yenye bei kubwa kuliko tanzanite, lazima wawekezaji watengeneze barabara ya kwenda na kutoka migodini ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa huduma za jamii,” amesema.

 

Viongozi wilaya, mkoa walaumiwa

 

Viongozi wa Mkoa wa Morogoro wanalalamikiwa kwa kile kinachodaiwa kuwa wamezuia ujenzi wa zahanati ili kumpisha mwekezaji katika Kijiji cha Epanko, Ulanga. Hatua hiyo inatajwa kuwaumiza wajawazito wanaohitaji matibabu.

Wanakijiji hao wameanza ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho, lakini umesimama kutokana na kuingiliwa na mradi wa utafiti wa madini unaoendelea kijijini hapo unaofanywa na kampuni ya Kibaran. Inadaiwa kuwa shughuli zote za maendeleo zimezuiwa kwa amri ya uongozi wa wilaya na mkoa.

Mkazi wa Kijiji cha Epanko, Pankras Kanyara, amemwambia Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko, kuwa kijiji hicho kilishatenga maeneo ya wawekezaji, lakini anashangaa kuona eneo lote la ardhi sasa linatumiwa na wawekezaji.

Anasema mwaka 2012 kampuni ambayo haikufahamika kwa wanakijiji hao ilianza uchumbaji Epanko na kuathiri vyanzo vya maji na hivyo kuibua mvutano kati ya wanakijiji na mwekezaji.

“Mwekezaji huyu tuliomba kukutana naye akakataa, tukaenda wilayani, alipoitwa aligoma mpaka alipoitwa mara ya pili. Alituambia kuwa ameshachimba nchi nyingi duniani…Baadaye akasema kwamba yupo hapa kwa ajili ya kufanya utafiti wa madini,” amesema Pankras.

Mwanakijiji mwingine, Syprian Kanyari, anasema wamekuwa wakinyanyaswa kwa kuweka mahabusu hata kwa miezi mitatu bila kufunguliwa mashitaka.

Anasema maendeleo ya kijiji yamedumaa, huku shule ya msingi kijiji hapo yenye wanafunzi zaidi ya 600 ina matundu manne pekee ya vyoo.

“Mkuu wa Mkoa amezuia hakuna ujenzi wa vyoo, wala kukarabati chochote mpaka kampuni ya mwekezaji sijui ifanyeje. Shule imekuwa magofu, walimu wanasafiri umbali mrefu kuja kufundisha wakati tulikuwa na uwezo wa kuwajengea hapa hapa,” amesema Kanyari.

Amemwomba Naibu Waziri amwulize rais kama anaridhia shule ifungwe kwa ajili ya mwekezaji.

Anasema mwekezaji wakati akafika Epanko alisema kuna aina saba za madini, na akadai kuwa magari yalisafirisha ‘mzigo’ wakati wote Serikali ikiwa haijui au kuchukua hatua zozote.

“Hivi serikali haina taarifa kama tunaibiwa? Tumeshaibiwa vya kutosha sana. Sisi wananchi wa Epanko tunaomba Serikali itutatulie kero zetu na umwambie rais kwamba tunakufa kila siku kutokana na zahanati yetu kukabidhiwa kwa mwekezaji,” amesema.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ulanga na Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Ulanga, Huluka Rajab amemwambia Naibu Waziri Biteko kuwa wilaya hiyo haijawahi kupata chochote kutoka kwenye madini yaliyopo Kijiji cha Epanko.

Dotto amemwuliza inakuwaje madini yenye thamani kubwa yachimbwe na wilaya isiambulie chochote, na akajibiwa kuwa wafanyabiashara hao huwa wanasaidia kutoa karatasi za kuchapia tu.

“Huwa wanatusaidia karatasi, pia waliwahi kusaidia madawati 40 tu hakuna kingine,” amesema Rajab.

Naibu Waziri wa Madini alikuwa kwenye ziara ya ukaguzi wa madini ya spino yanayochimbwa Kijiji cha Epanko, Wilaya ya Ulanga.

Kwenye ziara hiyo alikuwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Manya; Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga, Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wataalamu wa madini.

Naibu Waziri amekasirishwa na kitendo cha viongozi wa wilaya kwa kushindwa kufuatilia kampuni za uchimbaji madini Epanko na hivyo kuikosesha Serikali mapato makubwa.

“Haiwezekani madini yanachimbwa hapa kwenu, lakini hakuna kitu chochote mnachokifahamu. Madini yanasafirishwa na kuuzwa huko ninyi mpo hapa mmekaa na hamjali,” amesema.

Ameshangazwa na mwekezaji kampuni ya Kibaran kuelezwa kuwa na mtaji wa dola milioni 90 za Marekani, lakini ametoa soksi tu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Epanko.

“Madini yanayopatikana Epanko wala hayafanani na maisha ya wananchi wala mapato ya Serikali. Haya madini yamechimbwa miaka mingi, lakini Serikali imeambulia Sh milioni 22.52 kwa miaka mitatu tu. Hii haiwezekani kabisa.

“Wananchi wa Ulanga wametishwa hakuna anayethubutu kuzungumza, hatuwezi kuendelea hivi, bora tufunge biashara tunanze upya kuliko kuendelea na haya. Zipo kampuni zimetajwa, ni wajanja kupitiliza hivyo tumeamua kuchukua hatua.

“Tutafanya ukaguzi maalumu wa migodi yote na wafanyabiashara wa madini Ulanga. Hii ni tangu kuanza kuchimbwa kwa madini ya spino. Tutaangalia mapato, ushuru na mengine mengi,” amesema Biteko.

Amesema yeyote mwenye leseni ya uchimbaji madini anatakiwa kuandaa mpango wa huduma kwa jamii, hivyo ni sharti wenye leseni wote waandae mpango huo haraka.

Katika mazungumzo na JAMHURI, Biteko ameeleza masikitiko kuwa licha ya kuwapo taarifa zote hizo, bado mamlaka husika hazikuchukua hatua.

“Tunakwenda kufanya mashauriano ya ndani ili kuanza kazi ya pamoja na kufungua ofisi Ulanga na kwa usimamizi mzima wa madini. Wizara yetu ina watu wazalendo, hivyo sijapungukiwa na imani na wafanyakazi wetu wa madini waliopo,” amesema.

Amerejea mwito kwa wafanyabiashara wa madini akisema Serikali haiku tayari kuona wakifanya mambo kwa ujanja ujanja, na kuongeza kuwa kama kuna kipindi ambacho Watanzania watatajirika kwenye sekta ya madini, ni kipindi hiki kwa kuwa hakuna urasimu.

Amesema Tume ya Madini itachunguza na wale watakaobainika kukiuka sheria, Serikali haitasita kufunga migodi yao.

Kwa wale waliochimba madini Epanko na kuondoka bila kulipa ada stahiki, amewataka wajiandae kulipa madeni yote.

“Hatupo tayari kuona wafanyabiashara wa madini wakituchezea, kila aliyechukua mali atalipa,” amesema.

Ameulizwa ujasiri huo anaupata wapi, nay eye amesema, “Naupata kutoka kwa Rais Magufuli ambaye anapenda raslimali za nchi ziwanufaishe Watanzania wote, lakini pia ameonesha njia kwa kuchukia wizi, rushwa, ujanja ujanja na uhuni kwenye sekta ya madini. Pia Angella Kairuki ni Waziri asiyevumilia uhuni na wizi. Ni waziri anayejua kufuatilia kila kitu kwenye wizara na sisi tulio chini yake ametupa fursa ya kufanya kazi.”

Uchunguzi huu umefanywa kwa ushirikiano kati ya Gazeti la JAMHURI na Mfuko wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF).