Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Ndani, Hammad Masauni amesema kuwa wamebaini kuwepo kwa uanzishwaji holela na utitiri wa nyumba za ibada katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameyasema hayo yame leo Machi 26, 2024 wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Usajili wa Jumuiya za Kiraia itakayofanyika nchi nzima.
“Tumebaini uanzishwaji holelea wa nyumba za ibada katika maeno mbalimbali nchi jambo ambalo linaweza kuchangia kwa usumbufu hususan zilizo kwenye makazi ya watu,’ amesema.
Amesema baadhi ya jumuiya za dini hususan makanisa na misikiti yamebainika kujengwa katikati ya makazi ya watu na kusababisha kuwepo kwa mrundikano wa taasisi nyingi kwenye eneo dogo na baadhi ya taasisi kutumia sauti za juu na hivyo kusababisha adha na usumbufu katika jamii.
“Kutokana na hali hiyo sasa tunafanya usajili wa jumuiya za kiraia ili zile zinazoenda kinyume na sheria tutazifuta,”amesema.
Amesema changamoto zote hizo zinahitaji ushirikiano wa pamoja katika ushughulikiwaji wake, ili kuendelea kudumisha hali ya utulivu na usalama katika maeneo ya wananchi.