Na Mwandishi Wetu

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini na Taasisi zake imeweka mikakati ya kutangaza fursa zilizopo katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na ushiriki wake katika maonesho na makongamano ya kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha Sekta inakua na mchango wake kwenye Pato la Taifa unafikia asilimia 10 ifikikapo mwaka 2025.

Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo Julai 07, 2023 baada ya kutembelea banda la Wizara ya Madini na Taasisi zake na wadau wa madini kwenye kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa, kuongezeka kwa uwekezaji katika Sekta ya Madini kumetokana na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutangaza fursa za uwekezaji kupitia maonesho, mikutano na makongamano ya kimataifa.

” Na sisi kama Taasisi za Serikali tumejipanga kutumia maonesho haya kama jukwaa la kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini ili wananchi wengi waweze kushiriki kupitia shughuli za uchimbaji wa madini, biashara ya madini na utoaji wa huduma mbalimbali kwenye migodi sambamba na kufungamanisha na Sekta nyingine muhimu za kiuchumi.

Akielezea mchango wa wachimbaji wadogo katika Sekta ya Madini, Mhandisi Samamba amesema mchango wa wachimbaji wadogo kwenye ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali umeongezeka hadi kufikia zaidi ya asilimia 40 kutokana na mikakati mizuri iliyowekwa na Serikali katika kuwasaidia ikiwa ni pamoja na kuwapa leseni za uchimbaji wa madini na masoko na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa nchini.

Ameongeza kuwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umekua hadi kufikia asilimia 9.7 ambapo mikakati zaidi inaendelea kuwekwa ili kuhakikisha inazalisha ajira zaidi kwa watanzania na wawekezaji kupata faida na kulipa kodi na tozo mbalimbali Serikalini.