Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani
Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani imeandika historia mpya, ,baada ya Serikali kupitia Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) kuingia mkataba na Kampuni ya China Railways Seventh Group Limited kutekeleza ujenzi wa barabara ya Utete -Nyamwage km.33.7 .
Aidha Serikali kupitia wakala huo,imeingia mkataba na Kampuni ya Nyanza Roads Works ,ujenzi wa daraja la Mbambe M81 na barabara unganishi km 3.0 kwa kiwango cha lami , miradi ambayo itagharimu zaidi ya sh.Bilioni 67 hadi kukamilika kwake.
Zoezi la utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa barabara na Daraja hilo, uliofanyika viwanja vya Azimio Utete wilayani Rufiji Mkoani Pwani, umefanyika kati ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa barabara (TANROADS) Mhandisi Rogatus Matavila pamoja na Mwanasheria wa TANROADS Dorah Komba ,ikishuhudiwa na wananchi, viongozi mbalimbali na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya.
Akizungumza baada ya Zoezi hilo, Kasekenya alieleza, gharama za ujenzi wa barabara ya Utete-Nyamwage na Daraja la Mbambe zitagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.
Alieleza, ujenzi wa miundombinu ya barabara inakwenda kujibu kilio cha muda mrefu cha barabara ya Utete-Nyamwage kwa kiwango Cha lami ili kufungua maendeleo na uchumi wilayani Rufiji .
Hata hivyo,alisema, ujenzi wa miundombinu inaendelea kujengwa na kutanua mtandao wa barabara nchini ambapo hadi sasa zimeshajengwa km. 11,000 huku km.24,000 zikiwa bado zinahitaji lami.
Kasekenya aliiagiza TANROADS kusimamia ujenzi huo na kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuzingatia thamani ya fedha.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo , katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa barabara hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROAD) Mhandisi Rogatus Matavila alieleza, mkataba wa barabara ya Utete-Nyamwage ni moja ya mkakati wa Serikali kuharakisha maendeleo ya Rufiji ili kuboresha sekta ya usafiri na usafirishaji.
Matavila alielezea kwamba, upembuzi yakinifu wa barabara hiyo ulianza 2014 ambapo kutokana na muda kupita 2019 usanifu ulipitiwa upya .
Alifafanua, zabuni ilitangazwa Sept mwaka 2022 na kufunguliwa November 2022 na baada ya tathmini kukamilika ilishinda Kampuni ya China Bil 43.4 bila VAT na itajengwa kwa muda wa miaka miwili.
Akielezea kuhusu ujenzi wa Daraja la Mbambe Matavila alieleza, Daraja la sasa limejengwa kwa mbao ni jembemba lenye njia moja ya kupita magari na halina uwezo wa kubeba magari yasiyozidi tani tano na Lina miaka 30.
Alieleza, Daraja litakalojengwa litakuwa na njia mbili na upana wa mita 7.5 na upana wa Jumla mita 10.5 ,nguzo mbili za pembeni mwanzo na mwisho wa Daraja kukutana na barabara zote ili kuwezesha kupanda juu ili lisiathirike na maji.
“Ujenzi huo utaenda Sambamba uwekaji wa alama za barabarani na kuweka taa za barabarani solar lights 18 ambazo zitasaidia kulinda usalama wa watumiaji nyakati za usiku.”
Mbunge wa Jimbo la Rufiji, ambae pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii ,Mohammed Mchengerwa aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Utete-Nyamwage na amewaomba wakandarasi waanze ujenzi kwa kuanzia Utete hadi Nyamwage badala ya kuanzia Nyamwage kwenda Utete.
Alieleza, wanaRufiji walisubiri kwa kipindi chote ,na Sasa wanaishukuru Serikali kwa maendeleo yanayofanyika na kwenda Kuwa kitovu Cha maendeleo.
“Walipita viongozi mbalimbali kwa nyakati tofauti,na kila mmoja kuipigania Rufiji kadri ya uwezo wake na leo tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka miwili kutuletea Neema hii ya barabara ya Utete -Nyamwage kwa zaidi ya Bilioni 67”
Nae Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoani Pwani,Mwinshehe Mlao alieleza ,ujenzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM.
“Kwa hakika Leo nimefurahi sana kushuhudia jambo hili zito la uwekaji saini wa mikataba hii,namshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan,:;”Kwa muda mrefu jambo hili lilikuwa linatusumbua sana, tunaishukuru Serikali kwakuwa imetuweka pazuri kuweza kuzungumza na wananchi juu ya mazuri yanayofanyika “