Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dtk. Doto Biteko amesema kuwa Serikali itahakikisha inaweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji kwenye Sekta ya Nishati ili kuchochea maendeleo ya uchumi nchini.
Waziri Biteko ameyasema hayo, Oktoba 05, 2023 wakati alipokuwa akizindua ripoti ya utafiti wa ushirikiano kwenye sekta ya Nishati kati ya Tanzania na Sweden kwa miaka 60 pamoja na mambo mengine amesema kuwa Sweden imekuwa na mchango mkubwa sana kuisaidia Tanzania kwenye miradi mbalimbali ya Nishati hususani ya umeme.
“Sweden imekuwa ni moja ya nchini muhimu inayochangia kwa kiasi kikubwa kwenye miradi ya Nishati hususani umeme na imechangia shilingi bilioni 142 kwenye miradi ya ujazilizi kwenye vitongoji 1328 na Vijiji takriban 151 imechangia shilingi bilioni 52. Alisema Mhe. Doto Biteko
Aidha, kuhusu uwekezaji kwenye sekta ya nishati amesema kuwa kwa sasa wanajipanga kuongeza nguvu kwenye uwekezaji kwenye sekta ya nishati na kuwataka wadau wa sekta ya hiyo kuitumia vizuri fursa ya mikopo na misaada ya wadau wa maendeleo kama Sweden ili kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi.
Vile vile, Dkt. Biteko ameipongeza kampuni ya Scania kwa kuja na Teknolojia mpya ya kutumia taka ngumu kuzigeuza kuwa nishati ya kuendeshea magari na mitambo, hivyo taka zinazozalishwa hapa nchini zitageuzwa kuwa nishati ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Balozi wa Sweden Charlotta Ozaki alisema kuwa uhusiano wa ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden uliasisiwa na Rais wa awamu ya kwanza Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Waziri Mkuu wa Sweden kwa wakati huo na kusaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano hadi leo.
Balozi Charlotta alisema kuwa tangu ushirikiano huo uanze mwaka1963 hadi Leo 2023 tayari Sweden imetoa misaada ya takriban dola bilioni 8 kusaidia sekta ya nishati ikiwemo ujenzi wa miundo mbinu ya umeme na miradi ya umeme vijijini