Serikali ya Ufaransa imeporomoka baada ya Waziri Mkuu Michel Barnier kuenguliwa katika kura ya kutokuwa na imani naye.

Wabunge walipiga kura kwa wingi kumtaka aondoke, miezi mitatu tu baada ya kuteuliwa na Rais Emmanuel Macron.

Viongozi wa upinzani walileta hoja hiyo baada ya Barnier kutumia madaraka maalum kupitisha bajeti yake ambayo haikuwa imepigiwa kura.

Hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya Ufaransa kuanguka kupitia kura ya kutokuwa na imani tangu mwaka 1962.

Hali hii inaongeza msukosuko wa kisiasa nchini Ufaransa, ambako tayari uchaguzi wa mapema uliofanyika msimu wa joto ulisababisha ukosefu wa wingi katika upande zote bungeni.

Wabunge walihitajika kupiga kura ya ndio au kutoshiriki, ambapo kura 288 zilihitajika ili pendekezo lipite. Jumla ya kura 331 zilipigwa kwa ajili ya pendekezo hilo.

Barnier sasa anapaswa kujiuzulu kwa serikali yake na bajeti iliyosababisha kuporomoka kwake imepitwa na wakati.

Hata hivyo, anatarajiwa kusalia kama Waziri Mkuu wa mpito hadi Macron apate mrithi wake.

Mrengo wa kushoto na wa kulia walipeleka mapendekezo ya kutokuwa na imani naye baada ya Barnier kulazimisha mageuzi ya usalama wa kijamii kwa kutumia amri ya rais, baada ya kushindwa kupata uungwaji mkono wa kutosha.

Rais Macron, aliyerejea Ufaransa baada ya ziara rasmi Saudi Arabia, anatarajiwa kutoa hotuba ya kitaifa Alhamisi jioni.

Haathiriwi moja kwa moja na matokeo ya kura, kwani Ufaransa inampigia kura rais wake tofauti na serikali yake.

Macron alikuwa amesema hatajiuzulu vyovyote vile matokeo ya kura yatakavyokuwa.

Anatarajiwa kumteua waziri mkuu mpya haraka iwezekanavyo ili kuepusha aibu ya serikali isiyokuwapo – na zaidi, kwa sababu Rais mteule wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kuzuru Paris wikendi hii kwa ufunguzi wa kanisa kuu la Notre-Dame.