Katika pitapita yangu kwenye mitandao ya kijamii, nimekutana na uchambuzi ulionigusa kidogo. Nimebaini kuwa Baraza la Mawaziri linaongozwa na Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli (PhD – Chem&Maths), limejaa wasomi. Wasaidizi wake wakuu ni Makamu wa Rais: Samia Suluhu (Msc – Comm. EC. Dev.) na Waziri Mkuu: Majaliwa Kassim (B.A.Ed).

Ukiacha hiyo safu ya juu, linao maprofesa; Prof. Jumanne Maghembe, Prof. Makame Mbalawa, Prof. Sospeter Muhongo na Prof. Joyce Ndalichako. Wapo madaktari wa falsafa, Dk. Medard Kalemani, Dk. Augustine Mahiga, Dk. Ashantu Kijaji, Dk. Phillipo Mpango, Dk. Harrison Makyembe, Dk. Abdallah Posi na Dk. Suzan Kolimba. Pia wapo madaktari wa binadamu, Dk. Hussein Mwinyi na Dk. Hamis Kigwangala.

Si hao tu, wapo Wahandisi; Eng. Gerson Lwenge, Eng. Ramo Makani, Eng. Hamad Masaun, Eng. Isaack Kamwele, Eng. Stella Manyanya na Eng. Edwin Ngonyani. Wamo wenye shahada za uzamili za sayansi; Charles Kitwanga, January Makamba na Anastazia Wambula.

Wapo wenye shahada za uzamili za sheria; Ummy Mwalimu, Antony Mavunde, William Tate Ole Nasha

na Angella Kairuki. Wapo wenye shahada za uzamili za sanaa, ambao ni Mwigulu Nchemba, Jaffo Seleman, Angelina Mabula, Charles Mwijage na Nape Nnauye. Naye George Simbachawene anayo shahada ya kwanza ya sheria. Wawili; William Lukuvi na Jenista Muhagama wanaendelea na masomo ya shahada ya uzamili.

Kwa upande wa makatibu wakuu, wamo Prof. Kamuzora, Prof. Mkenda, Prof. Msanjila, Prof. Gabriel, Prof. Ntalikwa, Prof. Mdoe na Prof. Mchome. Wengine ni Dk. Ndumbaro, Dk. Mtasiwa, Dk. Mwinyimvua, Dk. Turuka, Dk. Mashingo, Dk. Budeba, Dk. Chamuluho na Dk. Yamungu.

Makatibu Wakuu wengine ni Dk. Kusiluka, Dk. Meru, Dk. Akwilapo, Dk. Ulisubudya, Dk. Pallangyo, Dk. Likwelile na Dk. Aziza. Wengine ni Eng. Itombe, Eng. Mwihava, Eng. Nyamhaga, Eng. Malingo, Eng. Futakamba na Eng. Emannuel.

Sitanii, nilipoona majina haya ya viongozi, moyo wangu ulipiga paaaaaa. Nikakumbuka Ibara ya 67.-(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosema; “Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo- (a) ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja, na ambaye anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza.”

Katiba hiyo hiyo, inasema mtu kuteuliwa kuwa waziri ni lazima awe mbunge. Kumbe kama sifa ya kuingia bungeni ni kujua kusoma na kuandika, kisha leo Rais Magufuli katika Baraza lake hajamchukua hata mmoja mwenye sifa hiyo, ni wazi mabadiliko ya haraka yanahitajika katika Katiba. Nashawishika kuwa muda wa majungu serikalini umekwisha.

Kauli mbiu ya Rais Magufuli ni HAPA KAZI TU. Najua umbea kwa watu wengine ni kipaji, ila katika hili napenda kuamini Baraza lake halitakuwa na muda wa kusogoa. Maprofesa hawa, wahandisi, madaktari, wanasheria, na wasomi wote waliosheheni katika Baraza hili katika ngazi ya uwazi na ukatibu mkuu naamini watachapa kazi.

Sitanii, naamini na natumaini hata Watanzania wenzangu wanaamini hivyo, kuwa wasomi hawa kwenye Baraza la Magufuli, hawakufika hapo kwa bahati mbaya. Hata kama kuna sehemu walikariri, ni wazi walielewa. Itakuwa aibu kubwa, tena aibu ya mwaka iwapo Baraza hili litashindwa kupuguza umaskini Tanzania.

Profesa Muhongo kitambo nilieleza alivyostahili kurejeshwa Wizara ya Nishati na Madini. Tayari tumeanza kushuhudia cheche zake akiwa Kanda ya Ziwa. Anaelekeza bei ya umeme ishuke na TANESCO waanze kufuata wateja. Rais Magufuli amejipambanua tangu mwanzo. Amesema Serikali yake itawahudumia wote bila kujali vyama vyao, itikadi zao, jinsia zao, wala rangi.

Nikiziangalia sura za mawaziri walioteuliwa, imani inakuwa kubwa. Sitaraji Waziri kama Profesa Ndalichako apate muda wa kusogoa, kusengenya au kupeleka majungu kwa Rais. Huyu tunamfahamu umahiri wake. Kiwango cha elimu walichonacho mawaziri hawa ni uhakikisho tosha kuwa Rais Magufuli naye anayo matarajio ya kweli kwao.

Nilipata kusema na hapa narudia. Mtu wa kumfanya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage aweze kufanya kazi yake vyema, basi anapaswa kuwa William Lukuvi. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lukuvi ndiye anaweza kuuondoa umaskini nchini Tanzania na kujenga matajiri wa kati.

Kwamba Lukuvi akiwezesha kila Mtanzania anayemiliki kipande cha ardhi kupata hati miliki, basi Watanzania hawa watakopesheka. Benki zitawaamini Watanzania, zitakuwa na uhakika kuwa fedha watakazowakopesha hazitapotea. Riba za mikopo zitashuka, Watanzania wengi wataweza kuifikia mitaji na wakipata mitaji watawekeza. Wakiwekeza, watajenga mitaji binafsi kutokana na faida wanayopata katika uwekezaji.

Sitanii, nafahamu fika kuwa Serikali hii ina kazi ngumu. Serikali hii inalo jukumu la msingi la kuondoa umaskini. Haiwezekani kuondoa umaskini bila kuwa na mikakati ya kweli. Naweza kuamini kuwa katika wakati huu Rais Magufuli yupo kwenye vita ya umaskini. Vita hii itafanikiwa kwa kuhakikisha Watanzania wote wanashiriki vita hii.

Yapo mambo yanaanza kujitokeza. Wapambe wanaanza vijimaneno. Nasikitika wanataka kutuhamisha kutoka mjadala wa kazi ya kukamua majipu na kutupeleka kwenye vijimaneno. Najua wapo waliokuwa wakinufaika na majipu anayokamua Rais Magufuli. Kwa sasa umeletwa mjadala mpya unaoanza kushika kasi. Wanataka Watanzania wahame kwenye umoja wa kupambana na umaskini waingie katika vita ya itikadi.

Nimeanza kusikia malalamiko kuwa baadhi ya watu ama wanaminywa katika sehemu zao za kazi au wanafanyiwa vitendo visivyo vya kiungwana ikiwamo kufukuzwa kazi. Haya yakianza kutokea, yatafungua uwanja mpya wa vita, watu watahama katika utumishi wa umma na kupambana na umaskini na kuelekea katika majungu.

Leo kwa mfano ikitokea Rais Magufuli akapata mpambe anayemwambia Hussein Bashe aliyekuwa msaidizi wa Edward Lowassa anamwangalia kwa jicho la kwa nini, hapana shaka kama akiingiza ubinadamu anaweza kuyaamini haya. Magufuli akiambiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la Rai enzi hizo, Muhingo Rweyemamu wakati Rais Benjamin Mkapa anabinafsisha nyumba za umma, leo ana hofu, linaweza kumwingia.

Sitanii, ikitokea Abdallah Majura Bulembo akamwambia Magufuli kuwa ‘anampakulia za jikoni’ za Lowassa, yampasa kufikiri mara mbili. Kwamba Bulembo huyu huyu aliyeshindwa Udiwani, akapata Uwenyekiti wa Wazazi kwa mgongo wa tunayemjua, akajiunga na kambi ya Pinda, hatimaye Magufuli, sisemi kuwa makini naye, bali kutekwa na kauli zake litakuwa janga la kitaifa.

Sitarajii ndani ya chama muanze kufukuzana baada ya uchaguzi eti tu kwa sababu fulani hakukuunga mkono katika hatua za uteuzi au mchakato wa uchaguzi. Nchini Marekani, Jenerali Collin Powel na Condoleezza Rais, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Rais George Bush, walimuunga mkono Barak Obama wa Democrat, lakini sikusikia wamefukuzwa ndani ya chama cha Republican. Unaufahamu mkondo ulioupitia kupata urais, hivyo usipoteze muda kufukua makaburi.

Serikali iliyopita ilijiendesha kwa vijembe na maneno ya kufikirika. Migogoro mingi ilianza kwa fukuto la ndani ya Serikali na chama kama vijimaneno vya kwenye khanga, lakini mara kadhaa ikaishia kuvunja Baraza la Mawaziri. Tafadhali Dk. Magufuli ukiletewa usivisikilize. Umeamua kuchapa kazi, hivyo usiruhusu watu wachache kuanza kukuletea vijimaneno.

Sitanii, Rais Magufuli mawaziri na watendaji hawa umewapata baada ya kuwachekecha mno. Ndiyo maana hukuona sababu ya kutowarejesha serikalini akina Ndalichako, Muhongo, Eliachim Maswi, Masauni na wengine waliokuwa wahanga wa umbea. Nakusihi uwe tayari kutetea mawaziri wako isipokuwa tu, itakapothibitika pasi shaka kuwa wanafanya ufedhuli. Ukiruhusu serikali yako kuvunjwa na Bunge kila wakati kupitia kamati mbalimbali, basi ujue hiyo miaka mitano itakwisha na ukigeuka nyumba hutaona kilichofanyika.

Kutoka kwa makatibu wakuu na mawaziri wako sasa uache kupokea mipango. Walazimishe mawaziri na makatibu wakuu kuleta taarifa za matokeo ya utekelezaji. Masuala ya mchakato, mpango mkakati, upembuzi yakinifu, kitanda cha barabara, mabega ya barabara, reli ya kati itakuwa ya kisasa, haya tumeyasikia sana. Kama maneno yangekuwa sehemu ya maendeleo Tanzania tungekuwa namba moja duniani.

Katika hili naomba kukukopesha mbinu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Akileta jungu kwako mtu, basi mwambie subiri kidogo. Mwite anyetuhumiwa na anayeleta tuhuma awepo kisha aseme wazi mbele ya huyo anayemtuhumu. Ukitumia utaratibu huu, hutopokea jungu hata moja. Watu watachapa kazi, utakuwa unaitwa katika uzidunzi wa viwanda, majengo ya kisasa, miundombinu ya reli, ndege na mabenki ya wazawa.

Rais Magufuli kama ulivyosema ni aibu sisi Watazania kushindwa kufanya biashara. Tumekuwa wachuuzi kwa kiasi kikubwa, badala ya kujenga viwanda tukasindika bidhaa na mazao, kisha tukapata masoko ya uhakika, tukalipa kodi, ajira zikawapo na mengine mengi yanayoweza kuisaidia nchi. Narudia, yeyote atakayekuletea jungu, mwambie asubiri wakati wa kampeni.

Sitanii, wakati nahitimisha makala hii niseme Baraza la Mawaziri na Makatibu Wakuu uliowateua ni wataalam. Nasisitiza. Itakuwa aibu kubwa iwapo hadi Baraza la Mawaziri linavunjwa mwaka 2020 Tanzania hii itakuwa bado dola inachezesha shilingi yetu, tunaagiza viatu kutoka nje ya nchi, tunauza pamba ghafi, kahawa hatukoboi wala kusaga, mahindi tunauza magunzi sokoni, n.k.

Wakati Rais Magufuli ukihangahika kukamua majipu kwa kukusanya kodi aweze kupata mtaji, nakuomba upitie sheria za uwekezaji kuweka mazingira rafiki kwa Watanzania wenye nia na uthubutu wa kuwekeza katika viwanda na biashara nchi hii ianze kutengeneza fedha hadi itoe msaada kwa majirani badala ya kusubiri kutembeza bakuli kwa wafadhili watujengee barabara na vyoo vya watoto wetu shuleni. Mungu ibariki Tanzania.