Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Serikali ya Jamhuri ya Korea imedhamiria kudumisha uhusiano mkubwa uliopo baina yao na Serikali ya Tanzania.

Hatua hiyo imekuja wakati taifa la Korea likiazimisha sikukuu yake ya taifa ambayo imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka.

Shughuli za maadhimisho hayo hapa nchini zilifanyika Ijumaa iliyopita ya Oktoba 4 katika hotel ya Hyatt Kilimanjaro hotel iliyoko jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo kwa hapa nchini yaliongozwa na balozi ya Korea hapa nchini AHN-Eun-Ju ambae alijumuika pamoja wageni waalikwa wengine wakiwemo wanadiplomasia na mabalozi huku mgeni rasmi ya shughuli alikuwa waziri wa habari, teknolojia na mawasiliano Jerry Silaa.

Waziri Silaa alihudhuria katika hafla hiyo akimuwakilisha rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt:Samia Suluhu Hassan .

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo waziri Silaa alianza kwa kuielezea siku hiyo kuwa siku muhimu katika historia na utamaduni wa jamhuri ya korea kwani inaashiria hatua muhimu katika mchakato wa maendeleo ya kijamii pamoja na kiuchumi.

Waziri Silaa ameeleza kuwa maadhimisho ya siku hiyo ni maadhimisho muhimu pia kwa serikali ya Tanzania inaakisi mabadiliko makubwa yaliyotokana na uhusiano mzuri kati ya taifa la Korea na Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo serikali kwa serikali na kubadilishana kati ya watu na watu.

“Tangu kuanzishwa kwa uhusiano wetu wa kidiplomasia , ushirikiano wetu umebadilika haraka hadi ushirikiano wa kisayansi. Tumeshuhudia mabadiliko hayo katika nyanja mbalimbali za ushirikiano iwe serikali kwa serikali na na kubadilishana kati ya watu na watu. Kwa hiyo, kwa wakati huu nitambue kwa shukran za uungwaji mkono wa serikali ya jamhuri ya Korea katika nyanja mbalimbali za ushirikiano ikijumuisha katika sekta za miundombinu, afya, maji, elimu, nishati, kilimo na teknolojia.”

Waziri Silaa ameongeza kuwa Tanzania imekuwa ikinufaika na misaada mbalimbali ya maendeleo ya korea ambayo imekuwa ikitolewa kupitia mashirika mbalimbali ya kimataifa.

“Muhimu zaidi Tanzania ni miongoni mwa wanufaika wa misaada ya maendeleo ya korea inayotolewa kupitia shirika la kimataifa la maendeleo la korea (KOICA) na mfuko wa maendeleo ya kiuchumi (EDCF). Misaada hii ni misaada na mikopo yenye masharti nafuu imekuwa misaada kwa serikali ya Tanzania katika kufikia ukuaji wa uchumi, kupunguza umaskini na kutekeleza malengo yote 17 ya ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu.”

Aidha waziri Silaa pia ameongeza kuwa waendelezaji wa Korea wamesaidia sana katika utekelezaji wa mpango wa tatu wa taifa wa masikio tano (FYDP III) ambao ni mpango wa mwisho kuelekea mwisho wa dira ya maendeleo ya Tanzania mwaka 2025.

Kwa wakati huu ambao taifa la Tanzania linaendelea na safari yake kuelekea kustawi kiuchumi, huku ikiendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wafanyabiashara na kujenga vitega uchumi ambavyo vitasaidia uchumi wa nchi kuwa mkubwa zaidi waziri Silaa alitoa takwimu za biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.

Kwa mujibu wa kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) takwimu hizo zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita (kuanzia mwaka 2014 mpaka agosti 2023) jamhuri ya Korea imewekeza dola za kimarekani millioni ishirini na nne na centi sabini(24.70 millioni) katika viwanda, utalii, kilimo, maliasili, ujenzi wa biashara na rasilimali watu ambayo imezalisha ajira mia tano na kumi na nane (518).

Akitoa takwimu waziri Silaa ametoa ripoti kuhusiana na upande wa biashara ambapo kwa mujibu wa shirika la mapato nchini (TRA) takwimu zinaonyesha kuwa kiasi cha biashara kiliongezeka kutoka shillingi za kitanzania billioni laki tatu na arobaini na nane, elfu mbili na mia arobaini na moja (348, 241 billioni) kwa mwaka 2017 na kuongezeka hadi shillingi za kitanzania billioni sita elfu sabini na mbili na mia saba na nne(672,704 billioni) kwa mwaka 2023.

Kupitia ziara rasmi ya Rais Samia Suluhu Hassan iliyofanywa mnamo mwezi juni mwaka huu nchini Korea, inatajwa kama miongoni mwa mambo ambayo yamechangia kuimarika kwa uhusiano baina ya taifa la Tanzania na Korea .

Rais Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya kikazi nchini Korea na kushiriki katika mkutano wa kwanza wa wakuu wa Korea na Afrika kwa mwaka huu 2024 kufuatia mwaliko wa rais wa Korea Suk-Yeol .

Kupitia ziara hiyo wakuu hao wawili walikuwa na mazungumzo ya pande mbili ambayo yaligawanya ushirikiano katika nyanja mbalimbali zikiwemo teknolojia, nishati na gesi, uchumi wa bluu, maendeleo ya miundombinu, afya, madini muhimu, biashara pamoja na uwekezaji.

Akizungumza waziri Silaa amesema kupitia ziara hiyo imefanikiwa kuboresha maeneo mapya ya ushirikiano kupitia mipangilio ya mfumo na makubaliano mbalimbali ambayo yalitiwa saini.

“Kupitia ziara hiyo tumeboresha maeneo mapya ya ushirikiano kupitia mipangilio ya mfumo na makubaliano ambayo yalitiwa saini ikiwa ni pamoja na mpangilio wa mfumo wa dola za kimarekani billioni 2.5 kwaajili ya miundombinu ya maendeleo kwa mwaka 2024 mpaka mwaka 2028.”

“Tunazingatia kwa shukrani ahadi za mikutano wa wakuu wa korea na Afrika kwa mwaka huu kwa ajili ya kuendelea kuunga mkono maendeleo ya Afrika kwa kuchangia dola billioni 10 hadi mwaka 2030. Ufadhili wa dolla billioni 14 kwaajili ya ufadhili wa mauzo kwa makampuni ya korea ili kuimarisha ushiriki wa makampuni ya korea katika maeneo hayo ya madini muhimu, uchumi wa bluu, biashara, miundombinu endelevu, mafunzo ya ufundi stadi na elimu, mabadiliko ya kidigitali pamoja na sayansi na teknolojia” Alisema waziri Silaa.

Kwa upande mwingine nae balozi wa Korea hapa nchini AHN-Eun-Ju amesema kuwa taifa la Tanzania ni mshirika kipaumbele wa Korea katika ushirikiano wa maendeleo hivyo Korea itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali.

“Tanzania ni mshirika kipaumbele wa Korea katika ushirikiano wa maendeleo. Kwa kuthibitisha hilo kuna baadhi ya mashirika ya maendeleo ya Korea yana ofisi za kikanda jijini dar es salaam ikijumuisha shirika la ushirikiano wa kimataifa la korea na benki inayosimamia utoaji wa mfuko wa ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi (Export-import bank).”

Aidha balozi huyo pia ameelezea kuhusu uungwaji mkono ubia wa kibiashara uliopo baina nchi hizo mbili huku akiyataja maeneo mbalimbali ya kiutalii ambayo yamekuwa ni ndoto za watalii wengi kutoka nchini Korea kufika sehemu hizo.

“Shirika la kukuza biashara na uwekezaji la korea linaunga mkono ubia wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili. Mashirika zaidi na zaidi ya korea kutoka sekta binafsi yanaonesha nia ya kufanya biashara nchini Tanzania. Serengeti, Kilimanjaro na Zanzibar ni vivutio vya ndoto kwa watalii wengi wa Korea”

Akiongeza balozi Ahn amesema kuwa wanatarajia kuona ongezeko kubwa la wingi wa mabadilishano ya kiutamaduni baina ya watu wa Korea na Tanzania kwani nchi zote hizo zina vipaji vya kutosha katika sanaa, sinema na muziki ambao unaweza kuleta watu kuwa kitu kimoja kupitia tamaduni zao.

Mbali na hayo balozi huyo alienda mbali pia na kuelezea namna ambavyo mipango ya misaada ya ruzuku ya Korea itakavyoinufaisha Tanzania huku ikilenga hasa maeneo ya vijijini.

“Mipango ya misaada ya ruzuku ya Korea inalenga wigo mpana wa wanufaika katika maeneo ya usafiri, elimu, afya, maji na usafi wa mazingira, kilimo na uboreshwaji wa fursa za kiuchumi kwa jamii za vijijini.” Alisema balozi Ahn.

Maadhimisho hayo ya sikukuu ya taifa la Korea yalienda sambamba pia na kuadhimishwa kwa miaka 32 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Korea ulioasisiwa mwaka 1992.

Shughuli hizo zinakuwa za kwanza kwa balozi mpya wa Korea hapa nchini Ahn -Eun-JU na kuwa ndiye balozi wa kwanza wa kike wa Korea nchini Tanzania.

Please follow and like us:
Pin Share