Mwaka huu, wakati Tanzania ikielekea kufanya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachounda Serikali, kimejidhihirisha kuwa hakina ubavu wa kudhibiti tatizo la rushwa nchini.

Hili limedhihirika katika uchaguzi unaoendelea wa viongozi mbalimbali wa CCM. Vitendo vya rushwa vimetajwa kuchukua nafasi kubwa kuwaweka watu madarakani bila kujali uadilifu na uwezo wao wa kuongoza.


Rushwa tunayoifahamu kuwa ni adui mkubwa wa haki, imedaiwa kutumika kama nyenzo kuu ya wagombea katika kushindana kwenye uchaguzi huo!


Kwa bahati nzuri wanaofichua siri ya rushwa katika uchaguzi huo ni wanachama wa CCM wenyewe wakiwamo wagombea walioshindwa katika vinyang’anyiro vya nyadhifa mbalimbali. Mifano ni mingi lakini miwili inatosha kuelezea.


Tumemsikia Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, akilalamika kwamba vitendo vya rushwa vilitawala katika uchaguzi wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara. Katika uchaguzi huo, Sumaye alishindwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu.


Pia tumemsikia Makongoro Nyerere akilalamika kuwa rafu ya rushwa iligubika uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara. Katika uchaguzi huo, Makongoro aliyekuwa akitetea kiti hicho aliangushwa na Christopher Sanya.


Wakati uchaguzi wa viongozi wa CCM ukielekea kuhitimishwa kwa kumchagua Mwenyekiti wa Taifa, wagombea wengi walioshindwa katika nafasi mbalimbali wameahidi kutoendelea kukaa kimya bila kuchukua hatua za kukemea matumizi mabaya ya fedha kwenye uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na kukata rufaa za kupinga matokeo husika. Lakini hizo zinaweza kuwa ni nguvu za soda tu!


Pamoja na tambo zake za mara kwa mara kwamba imejipanga kudhibiti kero ya rushwa katika uchaguzi kwa kutumia nguvu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), CCM imeendelea kuumbuka mbele ya wananchi kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake.

Hiyo ndiyo CCM, chama cha siasa kikongwe kinachotarajia kuchaguliwa tena kushika madaraka ya nchi, huku vyama vya upinzani, hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikikaribia kukipiku katika ushindani wa kisiasa nchini.


Tunatambua kuwa rushwa ni mdudu hatari mithili ya mchwa watafunavyo nguzo na mbao za paa kwenye nyumba. Wengine wanaifananisha rushwa na magonjwa hatari ya moyo, saratani, kisukari na ukimwi yanayopukutisha maisha ya maelfu ya watu kila siku duniani.

 

Kama CCM imekosa ubavu wa kudhibiti rushwa kwenye uchaguzi wake, Serikali itakayoundwa na chama hicho, itaweza kukabili tatizo hilo kwa uzito unaostahili? Ni ndoto za mchana kweupe!


Lakini cha kushangaza ni kwamba karibu wanachama wote wa CCM wanafahamu kuwa huwezi kupata uongozi ndani ya chama hicho bila kutumia fedha kushawishi wajumbe wakuchague. Kutokana na hali hiyo, karibu kila mgombea uongozi hujiandaa kutumia mtindo huo kuomba uongozi.

 

Kwa hiyo, ukiona na kusikia mgombea aliyeshindwa katika kinyang’anyiro cha nafasi fulani akilalamika kuchezewa rafu ya rushwa, ujue si kweli kwamba yeye hakutoa rushwa ila amezidiwa na rushwa iliyotolewa na mpinzani wake aliyemshinda. Huo ni ukweli usiopingika.


Basi, itoshe tu kusema kwamba Serikali ya CCM iliyo madarakani haijaonesha dhamira ya kweli ya kudhibiti rushwa katika uchaguzi na maeneo mengine yanayotoa huduma mbalimbali kwa wananchi.


Huo ni uthibitisho kwamba Serikali hiyo haitakuwa na jipya katika kushughulikia tatizo hilo hata baada ya kuongezewa muda wa kukaa Ikulu.

 

Vinginevyo, Serikali ya CCM itudhihirishie mapema kwa vitendo, uwezo wake wa kudhibiti rushwa kabla ya mlango wa hukumu (Uchaguzi Mkuu ujao) haujafunguliwa. Hatutaki kusikia utetezi kwamba muda uliobaki ni mfupi kwa Serikali kuonesha matokeo chanya ya juhudi zake katika kushughulikia kero hiyo.


Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema, “Wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza si kwamba rushwa haikuwepo, ilikuwepo lakini tulikuwa wakali sana. Ikithibitika mahakamani kuwa mtu ametoa au kupokea rushwa hatukumwachia hakimu nafasi ya kutoa hukumu peke yake.”


Kwa hali ilivyo sasa, viongozi wa CCM wanaonekana kujiweka kando katika mapambano dhidi ya rushwa, pengine wakiamini kimakosa kwamba jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa ni la Takukuru pekee.


Ndiyo maana viongozi wa CCM hawajaonesha dhamira ya kupiga vita rushwa kwa vitendo kukiwezesha chama hicho tawala kuwa mfano mzuri wa kuigwa nchini.


Ndiyo maana pia hatujaona wala kusikia wamekamatana kwa tuhuma za kutoa na kupokea rushwa kwa muda mrefu sasa.


Kwa upande mwingine, Takukuru nayo ni kama imedhamiria kuchangia anguko la CCM katika ushindani wa kisiasa nchini. Ninasema hivyo kwa sababu maofisa wa taasisi hiyo wamekuwa wakihudhuria mikutano ya uchaguzi wa chama hicho, lakini mara nyingi wamekuwa hawachukui hatua zinazostahili dhidi ya watoa na wapokea rushwa.


Ndiyo maana Fikra ya Hekima haisiti kusema kwamba taswira ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa viongozi wa CCM, inatushawishi wengi kuamini kuwa chama hicho hakina uwezo wa kudhibiti tatizo hilo katika siku za usoni. Labda kwa miujiza tu, maana nguvu ya Mungu haishindwi.