Shirika la Forum Syd Tanzania limeihimiza Serikali kuhakikisha inatimiza wajibu wake kwa kuwahudumia wananchi ipasavyo, na ameitaka na jamii yenyewe kuhakikisha inawajibika ili kuweza kukabili changamoto za umaskini wa kipato.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni jijini hapa na Mkuu wa Shirika hilo, Godfrey Wawa, katika mdahalo wa kujadili masuala mbalimbali yanayoikabili jamii ya Kitanzania.

 

Amesema Tanzania ina rasilimali nyingi, lakini inashangaza kuona Serikali na wananchi wanalalamikia suala la umaskini wa kipato.

 

Amefafanua kuwa tatizo linalosababisha umaskini nchini ni Serikali kutotekeleza wajibu wake ipasavyo kwa wananchi, huku wananchi nao wakishindwa kutambua wajibu na haki zao.

 

Amesema iwapo Serikali itawajibika ipasavyo kwa wananchi wake, na wananchi wenyewe kutekeleza wajibu wao kikamilifu, ni wazi kuwa suala la umaskini litapungua nchini kwa kiwango kikubwa.

 

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu cha Augustino (SAUT) kilichopo hapa, Imam Duwe, amesema wanawake ni wadau wakubwa katika uzalishaji mali na chakula, ambapo asilimia 70 ya chakula kinazalishwa kwa ushirikiano na nguvu za wanawake.

 

Kwa mujibu wa mhadhiri huyo, wanawake wanastahili kupewa ushirikiano mkubwa katika suala la uzalishaji mali, ili Taifa liweze kupiga hatua ya maendeleo ya kisekta.