Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Hatimaye Serikali imehitimisha mazungumzo baina yake na Jumuiya ya Wafanyabiashata nchini kwa kuafikiana kusimamia maazimio 15 huku ikitoa maagizo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)kusitisha mara moja mazoezi yote ya kamata kamata pamoja na mengine ya ufuatiliaji wa risisti za EFD.

Agizo hili linahusisha maeneo yote nchini hadi mwezi Agosti, 2024 ambapo pamoja na kusitishwa huko wafanyabishara wanahimizwa kuelendelea kutoa risiti za mauzo.

Ikumbukwe kuwa haya yanatokea ikiwa ni takribani siku nne kumekuwa na majadiliano kwa ngazi mbalimbali kati ya Serikali na viongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara hapa nchini yalitokana na madai na hoja takribani 41 ambazo wafanyabiashara waliziwasilisha serikalini ikiwa ni sehemu ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Thobias Makoba ameeleza hayo leo Jijini Dodoma, Juni 27, 2024: Saa 12:00 jioni kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu maadhimio ya kikao cha maridhiano baina ya Serikali na wafanyabiashara ambapo ameeleza kuwa kutokana na maazimio haya pande zote mbili zimekubakiana hali ya biashara kote nchini kuendelea kama kawaida ili kuwapa watanzania huduma wanazostahili.

Ameyataja maagizo mengine kuwa ni pamoja na kuweka mfumo mzuri utakaowezesha utoaji wa nyaraka muhimu za manunuzi wakati wa uingizaji wa bidhaa nchini kuanzia Julai, 2024 ambapo utekelezaji wake utawekewa utaratibu mzuri kwa kushirikisha wadau wote muhimu.

Pamoja na hayo amesema Serikali inaiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania kuongeza haraka Bandari Kavu (ICD) kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa mizigo kupitia utaratibu wa de-consolidation.

“TRA imeelekezwa kuongeza nguvu kwenye kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kodi na maboresho ya kodi yanayofanyika ili kuwezesha kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi nchini,Taasisi husika za Serikali pamoja na mabaraza ya biashara yashirikishwe kikamilifu katika ngazi zote, “amesisitiza

Amesema TRA pia inatakiwa kubainisha na kusimamia vyema orodha ya bidhaa nane ambazo zitawekewa bei elekezi kama ilivyo katika bidhaa za magari yaliyotumika. Bidhaa hizo ni vitenge, mashati, nguo nyingine, vipodozi, vito vya thamani, nguo za ndani, leso na vesti.

Makoba amesema Serikali kwa ujumla itaendelea na zoezi la kuwapanga na kuwawekea mazingira rafiki wafanyabiashara wadogo ambao hawako kwenye maeneo rasmi ili kurahisha usimamizi, ufuatiliaji na urasimishaji wao wa biashara.

“Katika kipindi cha muda wa kati, Serikali itaendelea kufanya mapitio ya viwango vya kodi tulivyo navyo kwa sasa ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa amani na haki kulingana na thamani ya biashara pia katika kipindi cha muda mfupi na wa kati, Serikali itashughulikia changamoto zote za wafanyabaishara zilizowasilishwa Serikalini hususan zile ambazo hazihitaji mabadiliko ya sera au sheria, “amesisitiza

Kuhusu maboresho zaidi, amesema Serikali inaigiza TRA ikamilishe maboresho ya mfumo wa TANCIS ambao utajumuisha moduli ya Auto valuation itakayoweka wazi na usawa katika ukokotoaji wa kodi kufikia Januari 2025.

“Wataalam wa TBS na TRA kwa pamoja wameelekezwa kukamilisha marekebisho ya mfumo wa TEHAMA ili mizigo inayoingia nchini kwa njia ya uchangiaji makasha iweze kugombolewa kwa namba ya usajili wa mlipakodi (TIN) ya mwenye mzigo badala ya TIN ya wakala bila ya kuwa na gharama za ziada kwa mlipakodi, zoezi hili linatarajiwa kukamilika Julai, 2024,”anafafanua

Kwa upande mwingine Serikali imeelekeza Wizara ya Fedha kuratibu zoezi la kufanya uchambuzi, tathmin na mapitio ya mfumo mzima wa utozaji na ukusanyaji pamoja na viwango vya Ushuru wa Huduma (Service Levy) pamoja na kushauri njia mbadala ya utozaji itakayo kuwa rafiki zaidi kwa wafanyabiashara ili kulinda mitaji na ukuaji wa biashara nchini.

Kuhusu wafanyabiashara kutoka nje ya nchi, Msemaji huyo amesema Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na mamlaka zingine husika itaendelea kuimarisha ukaguzi wa vibali vya kazi kwa wageni ili kuhakikisha kuwa wamiliki wa vibali hivyo wanafuata masharti ya vibali hivyo kwa mujibu wa Sheria za nchi.

“Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wanaokiuka Sheria, Kanuni, Taratibu na Masharti ya vibali vya ajira ikiwa ni pamoja na kuwafukuza nchini na waajiri husika kuchukuliwa hatua za kisheria, ” amesema

Amefafanua kuwa Mawaziri wanaohusika na sekta ya biashara watakutana na wafanyabiashara wote nchini kwa ajili ya kusikiliza changamoto za wafanyabiashara pamoja na kupokea maoni yatakayolenga kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini wakati wote.

“Wataalamu wa Forodha wakutane na Jumuiya ya Wafanyabishara nchini mara moja ili kujadiliana kuhusu taratibu za kiforodha hususani uthaminishaji na ugomboaji wa mizigo. Suala hili likamilike ifikapo tarehe 10 Julai, 2024,” amesema

Kutokana na maazimio haya na maagizo ya Serikali, pande zote mbili zimekubakiana hali ya biashara kote nchini kuendelea kama kawaida ili kuwapa watanzania huduma wanazostahili.