Na WMJJWM, JamhuriMedia, Arusha
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeimarisha uratibu na ushirikiano katika kutekeleza shughuli za utoaji wa huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia (MHPSS) nchini.
Hayo yamesemwa na Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Baraka Makona akifunga kikao cha kikosi kazi cha wataalam wa utoaji Huduma ya afya ya akili, msaada wa kisaikolojia na kijamii jijini Arusha.
Kamishna Msaidizi Makona amesema kuwa lengo kuu la kikao kikao kazi hicho lilikuwa ni kukutana kupitia maendeleo ya mpango kazi wa MHPSS nchini, kubadilishana uzoefu wa shughuli mbalimbali za MHPSS ndani ya na nje ya nchi, kupitia na kupanga kwa pamoja kalenda ya matukio na maadhimisho ya MHPSS kitaifa hivyo washiriki wakafanyie kazi yote waliyoyapitisha.
Kwa upande wake Mchungaji Elikana Gonda ameeleza kuwa ni wakati mzuri Serikali kutoa mwongozo kwa kushirikiana na viongozi wa dini utakaosaidia kutoa huduma hiyo katika jamii kwa kuzingatia taratibu na kanuni.
Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya akili (Mirembe) Dkt. Paul Lawala ameiomba Serikali kuongeza nguvu katika kuboresha vituo vinavyotoa msaada wa afya ya akili na msaada wa kisaikolojia nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwekaza huduma hiyo katika jamii ili kutokomeza tatizo la afya duni ya akili.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi Msaidizi, Huduma za Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais Tamisemi Dkt. Subisya Kabuje amekipongez kikosi kazi hicho hasa kwa kuheshimu umoja wa kupanga mikakati mizuri yenye tija Katika jamii hususan kutatua changamoto ya tatizo la afya duni ya akili na kutoa huduma ya msaada wa kisaikolojia.