Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha
Mamlaka ya serikali mtandao imetakiwa kuendelea kufanya tafiti ili kuleta bunifu za Mifumo ya TEHAMA ambayo sio tu itaboresha utendaji kazi bali pia itasaidia kuondoa kero za upatikanaji wa huduma mbalimbali za Serikali kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumisi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene wakati wa kufunga mkutano wa kikao kazi cha tano jana Jijini Arusha.
Waziri Simbachawene amesema agizo hilo linatokana na agizo la Rais alilolitoa kwa wizara hiyo kusimamia vyema matumizi ya Mfumo wa e-Mrejesho na kuhakikisha Taasisi zote za Umma zinatumia Mfumo huo katika kukusanya kero za wananchi zinazowasilishwa.
“Nitumie nafasi hii kuwakumbusha viongozi wa taasisi za Umma pamoja na watumishi kutekeleza agizo hili la Mhe. Rais, nasi kama Wizara tutachukua hatua kwa wale watakaokaidi agizo hili” amesema Waziri Simbachawene.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002505154-1024x683.jpg)
Vilevile imezielekeza Taasisi za Umma ambazo bado hazijahuisha taratibu za utendaji kazi wake (Business processes) kuhakikisha zinaandaliwa na kuwekwa kwenye maandishi ili iwe rahisi kujenga Mifumo inayowasiliana na kubadilishana taarifa kwa urahisi zaidi.
Pia ametoa rai kwa Taasisi zote za Umma ambazo bado zina kiwango kidogo cha utekelezaji wa Serikali Mtandao ziongeze kasi ya matumizi ya TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu yao na kuishirikisha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ili kwa pamoja itimize malengo ya kuijenga Serikali ya Kidijitali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya serikali mtandao Mhandisi Benedict Ndomba amesema Mamlaka itaendelea kushirikiana na Taasisi za Umma katika Kubuni, Kusanifu na Kujenga Mifumo mbalimbali ya TEHAMA itakayosaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii itakayowezesha Serikali kutoa huduma kwa wananchi kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu zaidi.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002505155.jpg)
“Niiombe Serikali kupitia Wizara yako kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu katika kuhakikisha Serikali ya kidijitali inafanikiwa zaidi” amesema Mhandisi Ndomba.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Mulula Mahendeka amesema kikao Kazi hicho cha siku tano cha Serikali Mtandao kimewakutanisha wadau zaidi ya 1,000 wa Serikali Mtandao kutoka katika Wizara, Mashirika na Taasisi za Umma ili kujadiliana na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002505158.jpg)