Kamati ya Bunge imeitaka Serikali ilipe deni la miezi 88 la Sh zaidi ya bilioni 3.145 inazodaiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, iliyosomwa na Dk. Mary Mwanjelwa kwa niaba ya Mwenyekiti wake, James Lembeli, imetaja taasisi za Serikali ambazo ni wadaiwa sugu.
Wadaiwa hao na kiasi cha fedha kikiwa kwenye mabano ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (mil 431.154), Wizara ya Miundombinu (mil 666.208), Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (mil 451.681) na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (mil 359.034).
“Kwa mara nyingine Kamati inaitaka Serikali kuhakikisha deni hili linalipwa haraka iwezekanavyo kama kweli inataka Shirika la Nyumba kukamilisha azma yake ya kujenga nyumba 15,000 ifikapo mwaka 2015,” imeagiza Kamati hiyo.
Kuimarisha utendaji kazi wa Shirika
Awali, Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Anna Tibaijuka, alisema ni azma ya Serikali kuhakikisha kuwa NHC inaendelea kuimarika.
Amesema mwaka uliopita Shirika liliendelea kuboresha muundo wake kwa kuwahamishia wataalamu wa fani ya ujenzi mikoani ili kuongeza kasi na ufanisi katika utekelezaji wa miradi.
“Katika mwaka 2012/2013, Shirika lililenga kuendelea na mchakato wa ununuzi wa ardhi yenye ukubwa wa ekari 26,887.9 katika Wilaya mbalimbali nchini. Hadi Aprili, 2013 Shirika lilikamilisha ununuzi wa ardhi yenye ukubwa wa ekari 1,210.6 na viwanja 457 na kuendelea na mchakato wa ununuzi wa ardhi yenye ukubwa wa ekari 18,421.
“Katika mwaka 2012/2013, Shirika liliweka lengo la kutayarisha miradi yenye nyumba 9,000 za makazi na biashara. Katika mwaka 2012/2013 NHC iliweka lengo la kuendelea kutekeleza miradi saba yenye nyumba za makazi 737 na kuanza utekelezaji wa miradi mingine yenye nyumba za makazi 4,114 zikiwa ni za gharama nafuu, kati na juu.
“Hadi Aprili, 2013, Shirika liliendelea na utekelezaji wa miradi saba ya ujenzi wa nyumba 564 za gharama ya kati na juu na kuanza miradi 11 ya ujenzi wa nyumba 642 za gharama nafuu. Katika utekelezaji wa miradi hii ya ujenzi, Shirika limekutana na changamoto mbalimbali zikiwemo zile za kutopata kwa wakati ardhi huru kwenye Halmashauri za Miji pamoja na vibali vya ujenzi.
“Kwa mwaka 2013/14, Shirika litaendelea kukamilisha miradi inayoendelea na kuanza miradi mingine mipya. Shirika litatoa kipaumbele kwa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu zisizopungua 20 kwa kila mkoa. Lengo ni kufikia nyumba za gharama nafuu zisizopungua 5,000 ifikapo mwezi Juni, 2015.
“Kulingana na Mpango Mkakati wa kipindi cha 2010/11 – 2014/15, Shirika linauza asilimia 70 ya nyumba za makazi zinazojengwa na kupangisha asilimia 30. Hadi Aprili, 2013, Shirika liliweza kuuza nyumba 386 katika miradi yake na kuliingizia Shirika Sh bilioni 23.3,” amesema Profesa Tibaijuka.