Nilipomuona Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudence Kabaka, akitengua uamuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) wa kuwataka madereva kurejea darasani, nilishangaa.
Nilikuwa miongoni mwa tuliopigwa na bumbuwazi kwa uamuzi huo, ingawa walikuwapo mamia kwa maelfu walioshangilia.


Uamuzi wa Serikali wa kukataa madereva kurejea darasani kusomea fani hiyo, umejidhihirisha sasa. Ndani ya miezi minne, wastani wa Watanzania 1,000 wamepoteza maisha katika ajali.  
Jamani, maiti za watu 1,000 si mchezo! Hata kama ungeweka miili ya kuku 1,000 lazima mtu ushtuke. Mbona hatushtuki? Mbona wenye dhamana hawajiuzulu ili kuonesha kuguswa na balaa hili? Hii ni idadi kubwa mno kuwahi kutokea katika nchi yetu, na pengine katika maeneo mengi ya Afrika na dunia.


 Idadi hii inaweza kuwa ni kubwa kuliko ile inayotokana au kusababishwa na Boko Haram kule nchini Nigeria na mataifa jirani. Watanzania tunaonekana wa ajabu kuyashangaa mauaji ya Boko Haram, lakini tukawa tunajiona tuna nafuu kwa mauaji haya ya barabarani.
Juzi tu, magaidi wa al Shabaab wameua watu 148 mjini Garissa. Kama ilivyo kawaida, Watanzania tumeonesha huzuni kubwa kwa mkasa huo. Nimejaribu kurejea kwenye kumbukumbu za magaidi wa al Shabaab sijaona idadi ya kuzidi watu 400 waliouawa ndani ya kipindi cha miezi minne.


Sisi ndani ya miezi minne wamekufa watu 1,000. Hatusikitiki kwa vifo vingi vingi, lakini tunasikitika kwa tukio la Garissa la watu 148!
Ninachojaribu kukisema hapa ni kwamba Watanzania tunakabiliwa na tatizo kubwa mno, lakini kwa sababu si tatizo la kusababishwa na mabomu au risasi, hatujitambui kama tuna hali mbaya. Hapa ni kama kipofu kuamini ana nafuu kuliko mwenye chongo.


 Nampongeza Mkurugenzi Mkuu wa NIT kwa sababu aliona mbali. Alitambua kuwa bila hawa madereva kurejeshwa madarasani, maisha ya Watanzania yatakuwa hatarini.
Msimamo wa NIT uliondolewa kisiasa. Mama Kabaka bila shaka alitumwa na wakubwa wake ili kumzima Mkurugenzi wa NIT. Wakubwa waliamua hivyo si kwa sababu wanawapenda sana wananchi, bali ni kwa kuwa waliona wanajiweka kwenye mazingira ya kukosa kura ifikapo Oktoba, mwaka huu. Utashi wa CCM unawatuma waamini kuwa kura za madereva zinaweza kuiangusha CCM!


Ndiyo hayohayo tuliyoyaona yakifanywa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kule Loliondo kwa kuamua kutengua uamuzi wa Waziri Khamis Kagasheki kwa sababu tu ndugu zetu wafugaji kadhaa walitishia kurudisha kadi za CCM kama Serikali ingeendelea na mpango wake wa matumizi bora ya ardhi.
Busara ya kawaida ingeitaka mamlaka ya juu kupima faida za madereva kurejeshwa darasani; kisha ikazilinganisha na hasara za kutofanya hivyo.


Kama tatizo lilikuwa gharama za masomo, hilo lingezungumzika. Kama gharama zilikuwa kubwa, kilichopaswa kufanywa ni kuzipunguza, lakini bado umuhimu wa madereva kurejea darasani ingebaki pale pale.
Ndugu zangu, uamuzi sahihi na madhubuti hauna budi kusimamiwa kwa gharama yoyote. Madereva waliogoma, waligoma wakitambua kuwa Serikali dhaifu ingesarenda na kutekeleza matakwa yao.


Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa hatuna Serikali inayosimamia uamuzi wake, hata kama uamuzi huo una manufaa makubwa kwa nchi na wananchi. Hakuna sababu ya kuwa kiongozi kama wanaoongozwa watakuwa ni watu wa kupinga kila lililo jema.
Nitatoa mfano. Mzazi mweledi hawezi kumkubalia mwanae kukataa kwenda shuleni kwa sababu tu siku hiyo mtoto kaamka na kilio kikali na kukitumia kama ngao ya kukaidi kwenda shule. Mzazi mweledi atamlazimisha mwanae aende shule, hata ikibidi kwa kumcharaza bakora. Atafanya hivyo kwa kupima faida na hasara za uamuzi wa mtoto wa kukataa kwenda shule.   


Mzazi dhaifu atasema: “Kama hataki kwenda shule, mwacheni abaki nyumbani.”
Serikali yetu imekuwa mzazi dhaifu ambaye anajua faida na hasara za mwanae kupata au kukosa elimu, lakini akawa hataki kumshinikiza kwenda shule. Watanzania tunapenda kulalamika na kurahisisha mambo.


  Vitabu vya filosofia vinasema hakuna kitu kinachoitwa bahati mbaya. Ajali si bahati mbaya. Ajali ni matokeo ya mambo mawili – uzembe na ujinga, basi! Ukiwa mzembe utapata ajali. Ukiwa mjinga kwa maana ya kutojua namna ya kukiendesha chombo cha moto au kusoma alama za barabarani, utapata ajali. Unapopata ajali katika mazingira na kwa sababu hizo mbili, hapo hakuna bahati mbaya.


Tena basi, Watanzania tumekuwa wepesi wa kumsukumia Mungu mzigo wa ujinga na uzembe wetu. Inapotokea ajali tumerahisisha mambo kwa kusema: “Ni mapenzi ya Mungu”. Mungu gani anayependa kuona roho za watu wake zikiangamia kwa ujinga na uzembe? Lini Mungu alitoa amri ya madereva wa Tanzania kutopenda kurejea darasani kuongeza maarifa?


Ndugu zangu, huku tunakoelekea, muda si mrefu, kila kazi itapaswa kufanywa na watu wenye weledi nayo. Tumefikia hatua sasa tuna wakata michongoma wanaojitangaza na kuonesha viwango vyao vya elimu. Tuna wasusi ambao kwenye matangazo wanaongeza na sifa yao muhimu ya “nina elimu ya ususi kutoka VETA”. Hawa hawafanyi hivi kwa sababu nyingine, isipokuwa wanasukumwa na ulimwengu wa ushindani. Wanafanya hivyo ili kuongeza mvuto.


Tupo kwenye kinyang’anyiro cha kazi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini kwa Afrika (SADC). Kuna vigezo vinawekwa vya madereva katika nchi hizo. Kuna vyuo vinavyoainishwa kwa ajili ya kumwezesha dereva au mwanataaluma mwingine kuweza kutambuliwa.


Madereva wa Uganda wanasoma. Madereva wa Kenya wanasoma. Rwanda, Burundi, Zambia, Msumbiji, Zimbabwe, Malawi kote huko wanasoma. Wanapasishwa kwa ajili ya kuwa na sifa za kuwawezesha kuendesha magari katika mataifa mbalimbali.
  NIT sijazungumza nao, lakini utashi wa kawaida unanifanya niamini kuwa wameliona hilo. Pamoja na kuhakikisha madereva wetu wanapata elimu ili kuokoa maisha na mali za Watanzania na watumiaji wengine wa barabara, wamelenga pia kuhakikisha Watanzania wanakuwa na sifa za kuendesha magari katika mataifa mengine.


 Kama uamuzi huu mzuri wa NIT unaweza kuwekwa kando kwa sababu za kisiasa, au kutafuta uhalali wa kuendelea kutawala, maana yake ni kwamba Serikali yetu inawaandaa madereva wa Tanzania kuishia ndani ya mipaka ya Tanzania. Kuna wakati utawadia ambao utawafanya madereva wa Tanzania kuishia Rusumo, Namanga, Sirari na kwingineko mipakani. Watalazimika kuishia hapo au kuyakabidhi magari kwa madereva wa huko wenye sifa. Sioni kwa utashi huu wa Serikali hii hii kama madereva wetu watamudu ushindani.


Tunaweza kufurahi hapa kwa kuwa na Serikali inayowaendekeza watu wanaodeka. Hiyo haina maana kwamba majirani zetu watakuwa na msamaha au huruma kwetu. Nasema kuwa kama kosa lilikuwa kwenye ada, hilo lingeweza kurekebishwa; lakini hoja ya msingi ya watu kurejea darasani ikabaki pale pale.  
Kwa kupuuza msimamo mzuri wa NIT, sasa tumekuwa wazoefu wa ajali. Hatushangai tena kusikia ajali ikiwa imeua watu 15, watu 20, watu 50 au zaidi. Ajali zimekuwa sehemu ya maisha yetu kiasi kwamba hata kwenye magazeti sasa habari ya watu 20 kupoteza maisha haipewi umuhimu wa kwanza.
Ajali zimekuwa sehemu ya maisha yetu kiasi kwamba hata Ikulu imechoka kupeleka salamu za rambirambi kwa wafiwa.


Kama nilivyowahi kuandika wiki kadhaa zilizopita, viongozi wakuu wa nchi wanaposhindwa kuguswa na ajali hizi, tusitarajie muujiza. Kama wanaweza kufa watu 50 katika ajali na asionekane Waziri au Rais katika eneo la tukio, tusitarajie kupungua kwa maafa haya.
Kwangu mimi bado naamini Mkurugenzi Mkuu wa NIT ataendelea kuwa sahihi kwa uamuzi wake alioufikia na baadaye ukapanguliwa na wasaka sifa za kuwawezesha kupendwa na wapigakura.


Serikali ijayo iwe ngumu. Isimamie kile inachokiamini. Iijenge Tanzania kwa manufaa ya Watanzania wa sasa na wajao. Kuna mambo mengine hata kama ni machungu, ni lazima tuyatekeleze kwa ajili ya kuijenga Tanzania imara.
Uongozi si kazi ya kumfurahisha kila mmoja. Angalia, leo madereva wamefurahishwa kwa kuzuiwa kurejea darasani, lakini angalia vilio vilivyotamalaki nchini kutokana na udhaifu wa madereva wetu.


Serikali iwe imara. Inapoamua jambo, ilitekeleze hasa kama inaamini kuwa jambo hilo lina manufaa kwa wengi. Kama madereva wanagoma, Serikali itambue kuwa nchi hii haina uhaba wa watu hao. Jeshini wapo. Polisi wamejaa tele. Kama tunashindwa kupata idadi ya kutosheleza, wapo Wakenya wengi hawana kazi za udereva licha ya kuwa na sifa zinazotakiwa.   


Milango ifunguliwe ili wenye sifa kutoka ughaibuni waje wafanye kazi hiyo. Kama Wachina wanauza mahindi ya kuchoma, sioni ni kwa namna gani watashindwa kuja kukamata ajira za udereva za Watanzania wasiotaka kwenda darasani.
Kama ilivyo kwa mzazi anayemlazimisha mwanae kufanya jambo lenye manufaa kwake na kwa jamii yake hapo baadaye, Serikali yetu nayo inapaswa kufanya vivyo hivyo. Kuruhusu kutofanyika kwa jambo jema, hata kama tunajua faida ya jambo hilo, si udhaifu tu, bali ni dhambi pia.


Serikali makini lazima isukume mbele baadhi ya mambo magumu hata kama kutakuwapo upinzani wa hapa na pale. Serikali ya kusarenda kila inapotishwa, si Serikali inayotakiwa na Watanzania ifikapo Oktoba, mwaka huu.