Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma
Serikali imetangaza kuzifunga laini za simu zaidi ya milioni mbili ambazo hazijahakikiwa licha ya Serikali kuhimiza wananchi kuhakiki laini zao.
Hayo yamebainishwa leo Januari 24,2023 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma.
Waziri Nape amesema kuwa hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa utapeli ambapo kwa mujibu wa takwimu za Januari 19, mwaka huu, zaidi ya laini milioni 60 zimesajili huku zilizohakikiwa ni milioni 58.
“Sababu ya kuzifungia laini hizo ni kuondoa utapeli uliopo hivi sasa kupitia simu za mkononi kwani laini zinazotumika ni zaidi ya milioni 60 katika watu milioni 61 tuliopo hapa nchini.
“Eneo hili la mawasiliano linagusa watu wengi lakini hata hivyo kuna utapeli mwingi ndio maana tuliposema watu wafanye uhakiki ni laini milioni 58 tu ndiyo zilisajiliwa na zaidi ya milioni mbili hazijahakikiwa.” amesema.
Hata hivyo amesema Serikali imeongeza muda wa kuhakiki laini zao kutoka Januari 31, mwaka huu, hadi Februari 13, mwaka huu, ili kutoa nafasi zaidi kwa watu kuhakiki laini zao.
“Zipo laini nyingi mtaani na nyingi zinatumika katika utapeli ,wapo mawakala wasiokuwa waaminifu kwani wanahifadhi namba na picha za watu wenye namba za NIDA na kuwasajilia watu wengine huku muhusika mwenyewe akiwa hajui kama jina lake linatumika na watu wengine na nyingine ndiyo hizo zinatumika katika utapeli,hivyo tutazima laini zote zilizosajiliwa kwa uongo lengo kubwa ni kuondoa utapeli.,” amesema.