Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekusudia kuwekeza katika Makazi ya Wazee nchini ili kuwa na miradi mbalimbali itakayozalisha mazao na kuchangia katika mapato ya Serikali.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wakati akizungumza na waandishi wa Habari mkoani hapa mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kukagua huduma zinazotolewa na Makazi ya Wazee katika mikoa ya Singida, Manyara, Kilimanjaro na Morogoro.
Amesema kuwa ziara hiyo imefanyika kimkakati ikiongozwa na Waziri wa Wizara hiyo, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na wataalam wengine wa Wizara imelenga kukagua huduma zinazotolewa katika Makazi 14 yenye Wazee 271 yanayosimamwiwa na Wizara ili kuweka mikakati na mbinu mbalimbali zitakazosaidia makazi hayo kuwa na huduma bora na kuwekeza nguvu katika miradi mbalimbali ya kilimo, mifugo na uzalishaji mali katika makazi hayo.
Akizungumza kuhusu uwekezaji wa miradi ya maendeleo katika Makazi hayo nchini amesema mfano Makazi ya Wazee Fungafunga yenye ekari 10 inaweza kutumika katika shughuli za kilimo cha mbogamboga, ufugaji wa kuku na miradi mingine ya kimkakati.
“Makazi haya ndio tunatoa huduma kwa wazee wasiojiweza na wasio na ndugu ila hamkatazwi kuzalisha hapa nilipo katika Mkazi haya ya Wazee Fungafunga Afisa Mfawidhi wa hapa amekuwa mbunifu na kutumia eneo kulima mbomboga zinazosaidia wazee na pia kuongeza kipato” amesema Dkt. Chaula.
Aidha ametoa rai kwa jamii kuwajibika katika malezi ya wazee kwani sehemu salama na ya kwanza ya wazee ni katika familia zao ili waweze kupata huduma bora na uangalizi mzuri kutoka kwa ndugu na familia zao.
Pia alisisitiza wananchi kujitokeza kuhesabiwa tarehe 23/08/2022 ili kusaidia kupata takwimu sahihi hasa za wazee nchini kwa ajili ya kusaidia kuweka mikakati stahiki ya kuwahudumia wazee katika utoaji wa huduma hasa za Afya na huduma nyingine muhumu kwa wazee.
Akitoa taarifa ya Makazi hayo Afisa Mfawidhi Rehema Kombe amesema wamekuwa wakizingatia taratibu zote katika kuhakikisha wanapokea wazee wenye mahitaji hasa katika Makazi hayo na kutoa elimu kwa jamii kwa kushirikiana na Manispaa ya Morogoro kutunza Wazee katika familia zao.
Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa Mzee Lameck Sendo alisema Baraza la Ushauri la Wazee Taifa kazi yake ni kuishauri Serikali hivyo wameishauri Serikali kuboresha mazingira ya Makazi ya kulea Wazee wanayoyasimamia ili wazee wasiojiweza na wapate huduma bora na kuhimiza viongozi wa Baraza hilo katika ngazi ya kata mpaka mikoa kuwatembelea wazee katika Makazi hayo na kuwapa faraja na misaada mbalimbali.
Naye mmoja wa Mzee anayehudumiwa katika Makazi ya Wazee Fungafunga Mzee Osea Daniel Mganga ameiomba Serikali kuendelea kuboresha huduma katika Makazi hayo hasa katika miundombunu akitolewa mfano barabara ya kuingia katika makazi hayo ikiwa na changamoto hivyo ikitengenezwa itasadia kutoa huduma za dharura katika makazi hayo ikiwemo zimamoto na magari ya wagonjwa kufika kwa urahisi.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ikiongozwana Waziri wake Dkt. Dorothy Gwajima Naibu wake Mwanaidi Ali Khamis, Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula, Naibu wake Amon Mpanju na wataalam wengine wa Wizara hiyo wametembelea na kukagua huduma zinazotolewa katika Makazi ya Wazee na Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara kwa lengo la kujifunza, kusikiliza changamoto mbalimbali ili kuzipatia ufumbuzi na kuboresha huduma kwa wananchi