Na Catherine Sungura, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali itaendelea kuweka mkazo wa kipekee katika kusukuma maendeleo vijijini kama njia sahihi ya kuchochoa uchumi jumuishi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo wakati wa kupitisha Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2024/2025 na Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Prof. Mkumbo alisema suala la kuweka mkazo katika maendeleo vijijini tayari wanayo mifano ya msingi ikiwemo TARURA ambapo mtandao wa barabara za vijijini umeongezeka kwa mwaka 2020 hadi 2024.
Alisema serikali kupitia TARURA imefanikiwa kuongeza kiwango cha barabara za changarawe kutoka Km. 24493 hadi kufikia Km. 41107 mwaka 2024 ikiwa ni zaidi ya lengo.
“Lengo letu ilikuwa ni kufikia Km. 35000 ifikapo mwaka kesho lakini tayari tuna mtandao wa Km. 41107.52 kupitia TARURA, kwenye lengo la kuwezesha watu wetu kupata kipato, kufanya biashara suala la barabara vijijini ni muhimu sana”.
“Tukishakuwa na mtandao wa barabara vijijini hii maana yake itasaidia wananchi kuweza kufanya biashara, kusafirisha mazao yao ya mifugo, kilimo, uvuvi na kadhalika kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na kujipatia kipato”, aliongeza.
Vilevile alisema kwamba kiwango cha barabara kimeongezeka kutoka Km. 2205 mwaka 2020 mpaka Km 3224 mwaka 2024 na kwa miradi inayoendelea na anaamini hatua kubwa zaidi itaongezeka.