Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Arbert Chalamila amesema Serikali itawalinda wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo waliofungua maduka yao siku ya leo licha kuwepo kwa mgomo.
Chalamila ameyasema hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa eneo hilo la Kariakoo, ambapo maduka mengi yamefungwa kufuatia mgomo wa wafanyabiashara ulioanza leo Juni 24, 2024.
“Mliofungua maduka hongereni na hakuna yeyoye atakayewasumbua…nataka niwathibitishie yule atakayemletea mkwara aliyekubali kufungua, naapa mbele ya Mwenyezi Mungu hapo ndipo nitakapoonyesha ‘show’ nzima,” amesema.
Amesisitiza kuwa madai ya wafanyabiashara hao yanashughulikiwa na Serikali na hivi sasa viongozi wa wafanyabiashara hao wapo mkoani Dodoma kwa mazungumzo na viongozi wa Serikali.
“Hebu niwaulize swali ndugu zangu, Sasa ikatokea mambo hayo yakachukua mwezi mzima na mimi nikasema askari wangu wote watalinda eneo hili hakuna mtu tena kufungua duka mpaka tutakapo suluhisha, kwa mwezi mmoja itakuwa sawa au sio sawa.
“Nyie mnafikiri mimi nikatuma vikosi vilinde hapa kuna mtu atainama afungue hapa? Mimi nikasema nianzishe vita masaa mawili hapa… Kwahiyo lazima kwenye biashara tuwe na uvumilivu ambao unaweza ukatufikisha tukaishi salama kuliko tulivyokuwa jana,” amesema na kuongezwa:
“Tanzania hii ni ya kwetu sote. Kwahiyo Mimi cha kwanza nilichopita hapa ni kuwaambia hongereni na asanteni mliokubali kufungua maduka na nyie ambao mmeendelea kufungua nawathibitishia kwamba nitazilinda Biashara zenu wala hakuna mwizi atakayeziiba…mkitaka kufunga Kwa mwezi sawa wakati sisi tunaendelea kushughulikia yale mliyoyapeleka,”.
Wafanyabiashara hao wamefunga maduka Kwa madai ya kuchoshwa na vitendo vinavyofanyiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).