Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali imebaini uchanganyaji wa bangi yenye kiasi kikubwa cha kilevi katika vyakula vikiwemo biskuti, asali, juisi, majani ya chai na keki na kueleza kuwa itawachukulia hatua wote watakaobainika.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, amesema hayo leo Mei 30,2023 jijini Dodoma hapa wakati akitoa taarifa ya hali dawa za kulevya ya mwaka 2022.

Ameitaja mikoa inayoongoza kulima bangi kuuza nje ya chi ni Arusha, Iringa, Morogoro na Manyara huku mikoa ya Mara na Ruvuma ikiongoza kulima kwa matumizi ya ndani.

“Tukiangalia Taarifa ya Dunia ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2022 utaona kuwa asilimia 40 ya nchi zenye matumizi makubwa ya bangi, zilikumbwa na idadi kubwa ya magonjwa ya afya ya akili, uhalifu, uvunjifu wa amani uliosababishwa na matumizi ya dawa hizo,” anasema.

Waziri huyo amefafanua kuwa bangi imeendelea kuwa ni dawa inayotumika zaidi nchini licha ya juhudi za serikali za kutaka kutokomeza matumizi ya dawa hiyo ya kulevya.

Amesema mwaka 2022, serikali ilifanikiwa kuteketeza hekari 179 za mashamba ya bangi na tani 20.58 za dawa hiyo ambazo zilikamatwa katika mwaka huo.

Ameongeza kuwa katika operesheni za ukamataji wa dawa za kulevya zilizofanyika nchini kwa mwaka 2022, zilifanikisha kukamata tani 15.2 za mirungi, kilo 254.7 za heroin na kilo 1.7 ya cocaine.

“Kumekuwepo na mwendelezo wa ukamataji wa dawa ya kulevya aina ya methamphetamine ambapo kwa mara ya kwanza mwaka 2021 4 zilikamatwa kilo 430.8 na kufuatiwa na gramu 968.7 ambazo zilikamatwa mwaka 2022,”anasema.

Amebainisha kuwa katika kukabiliana dhidi ya wimbi la matumizi ya dawa za kulevya, serikali imeendelea kufadhili mafunzo ya stadi za kazi kwa waraibu wanaopata nafuu.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2022, waraibu 245 waliopata nafuu waliunganishwa katika vyuo vya VETA na Don Bosco kupapata ujuzi wa kujiajiri ili wasirejee kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

Waziri Mhagama amewataja wananchi wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kilimo cha bangi na mirungi kuacha mara moja.

Amesena kuwa serikali itahakikisha wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu, watatafutwa popote walipo na kukamatwa kisha kufikishwa katika vyombo vya sheria.