WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema serikali ina mpango wa kuanzisha chombo cha kuratibu na kusimamia mikataba ambayo serikali inaingia.
Hatua hiyo ya kunusuru nchi kuingia katika mikataba yenye masharti hasi na inayoigharimu serikali.
Amesema hayo wakati wa kufungua kikaokazi kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari na wakurugenzi na wakuu wa vitengo vya sheria katika wizara, taasisi za umma na mamlaka za serikali za mitaa ambao ni zaidi ya 300.
Amesema moja ya udhaifu uliopo ni usimamizi wa mikataba baada ya kuwa imesainiwa.
Amesema akiwa kwenye timu maalumu ya majadiliano ya rais katika kipindi cha miaka saba, walibaini baadhi ya watendaji wa taasisi za serikali kutokuwa na uelewa wa namna ya utekelezaji wa baadhi ya masharti yaliyomo katika hati za makubalino yaliyofikiwa baina ya serikali na wawekezaji, hivyo kuwatia hofu wawekezaji.
Amesema pia walibaini uchache wa wataalamu mahiri na wabobezi wa majadiliano katika maeneo mbalimbali ya majadiliano. Profesa Kabudi amesema walibaini pia weledi unaohitajika kubaini ujanja, mbinu na hila za ukwepaji kodi, uhamishaji wa faida kwa kutumia mitandao ya kampuni yaliyoundwa katika maeneo ambayo ni mahususi kwa ukwepaji wa kodi na uhamishaji wa faida.
Walibaini uvamizi wa maeneo ya leseni au maeneo ya ardhi na kuingia makubaliano na wawekezaji kwa lengo la kulipwa fidia kwa mtindo wa tegesha na kusisitiza kuwa kuna mashauri mengi katika eneo hilo.
Amesema eneo lingine walilolibaini ni kampuni kusisitiza kutumia mahakama za nje kwa masuala ya usuluhishi wa migogoro na kuwataka wanasheria wa serikali kutoa maelezo ya kutosha kuwa mashauri kama hayo pia yanaweza
kufanyika nchini.
“Ili kuondokana na changamoto hizo, tulishauri kuwa ni vyema serikali kuwa makini kutekeleza makubalino ya kimkataba na kuona umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika majadiliano na huu ndio msingi wa kuja na mpango wa kuanzishwa chombo cha kuratibu na kusimamia mikataba,” amesema.
Amesema kuanzishwa kwa chombo hicho kutaisaidia nchi kubaini mapema migogoro ya kimkataba na kuitafutia njia ya kuyamaliza bila kwenda mahakamani.
Profesa Kabudi amewataka mawakili wa serikali kutumia sheria zinazosimamia maslahi ya taifa kuzitumia kama miongozo wakati wa kufanya majadiliano na kuandaa mikataba ili isiwe na masharti hasi.
Kwa upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johari alisema pamoja na mambo mengine, wataalamu wabobezi wa sheria kutoka Uingereza watatoa mada kuhusu ushirikishwaji wa mashauri ya kimataifa ya usuluhishi, mikataba ya kimataifa ya uwekezaji na vihatarishi vilivyopo kwenye sheria za uwekezaji.