Na Munir Shemweta, JamhuriMedia, Rorya
Serikali itatoa fidia ya kifuta jasho cha maendelezo kwa wananchi watakaobainika kuvamia eneo la shamba la Utegi lililopo wilayani Rorya mkoani Mara baada ya kufanyiwa utambuzi.
Eneo lililovamiwa lina ukubwa wa hekta 476.52 na kujumuisha vitongoji vya Kibinyongo, Mabatini, Oringa, Denga na Omuga ikiwa ni pamoja na eneo la shule ya msingi Utegi iliyopo karibu na ofisi za utawala za shamba.
Aidha, uongozi wa wilaya ya Rorya umesitisha mipango ya kuboresha miundombinu ya shule ya msingi Utegi ya kujenga majengo na matundu ya vyoo licha ya kiasi kikubwa cha fedha kupelekwa kwa ajili ya kusubiri nchakato wa kuhamisha shule hiyo kupisha shughuli za shamba.
Hayo yamebainishwa tarehe 7 Mei 2023 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipokwenda kutoa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na mgogoro wa matumizi ya ardhi baina ya wananchi na shamba la Utegi katika halmashauri ya Rorya mkoani Mara.
Pamoja na kutambua uvamizi uliofanyika ndani ya shamba hilo, Dkt Mabula aliwaeleza wananchi kuwa, serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kulipa kifuta jasho kwa kulipa fidia ya maendelezo kwa wananchi watakaobainika kuvamia shamba hilo.
Alisema, zoezi la uthamini wa maendeleo ya wananchi litafanywa kwa njia shirikishi likihusisha wathamini kutoka mkoa wa Mara pamoja na wizarani.
“Timu ya wataalamu imeandaa mpango kazi na bajeti ya kuendesha zoezi la uthamini na serikali itahakikisha kuwa zoezi hili linatekelezwa kwa uwazi mkubwa na linakuwa shirikishi kwa wananchi wa ngazi zote” alisema Dkt Mabula.
Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema kuwa, serikali itazingatia maslahi mapana kwa wananchi ikiwemo kuhakikisha ulinzi na usalama wakati wote wa zoezi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, utekelezaji wa uamuzi wa Baraza la Mawaziri juu ya migogoro ya matumizi ya ardhi utaimarisha usimamizi wa maeneo mbalimbali ya serikali, ukuaji wa uchumi pamoja na kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao.
“Ukamilishaji wa zoezi hili kwa wakati utasaidia kuzipatia ufumbuzi kero za wananchi na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za nchi”. Aliongeza Waziri Mabula.
Shamba la Utegi ni eneo la shamba lililotumika kwa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa lengo la kupata malighafi ya maziwa ya kiwanda pamoja na kuzalisha mitamba (ng’ombe bora wa maziwa) kwa ajili ya wananchi wa maeneo yanayozunguka shamba.
Eneo hilo lilitwaliwa kutoka sehemu ya vijiji 6 vya Utegi, Mika, Omuga, Nyasoro, Nyanduga na Igri ambavyo vinaunda umoja wa vijiji ujulikanao kwa jina la UMONI mwaka 1969 ambapo lililimwa kama shamba la mifugo Utegi .Na. 168 mwaka 1974 likiwa na ukubwa wa hekta 5.048.02.