Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini.
Rais Samia ameyasema hayo leo Julai 03, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (DITF) maarufu Sabasaba yaliyofunguliwa rasmi na Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi.
“Ndugu wafanyabiashara serikali itaendelea kufanya Kila linalowezekana kusikiliza na kutatua changamoto za Wafanyabiashara nchini.
“Mfanyabiashara yeyote mwenye maoni ya kuboresha, Kujenga na kusaidia nchi milango ipo wazi waendelee kuwasiliana na Mamlaka zetu mbalimbali ikiwemo Wizara yenye dhamana ya Viwanda na Biashara bila kusahau Taasisi yake ya Tantrade,” amesema Rais Dkt. Samia.
Aidha Rais Dkt. Samia amesema kuwa mauzo ya nje ya bidhaa za zetu nchini yalipanda kutoka Sh. Trilioni 12.3 mwaka 2019 hadi kufikia Sh. Trilioni 17.3 sawa na dola za Marekani bilioni 6.56 mwaka.
Amesema serikali itaendelea kujenga, kuboresha na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya miundombinu ili kuhakikisha wanaongeza tija kwa uzalishaji kwa wingi na sifa.
“Tutakamilisha miradi ya miundombinu ili bidhaa zinazozalishwa ziweze kufika kwa urahisi kwenye masoko yaliyokusudiwa,” amesema Rais Samia.
Aidha Rais Samia amesema maonesho hayo ya sabasaba kwa mwaka huu yamezikutanisha zaidi ya kampuni 3486 ya ndani nan je ya nchi na kwamba hiyo inaonesha ukuaji na mvuto wa jambo hilo.
“Mvuto huu umechangiwa na juhudi za serikali katika kusimamia misingi imara na thabiti kwenye kujenga uchumi jumuishi na shindani kiwenye nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, viwanda na uwekezaji.
“Ni ukweli usiopingika njia moja wapo ya kufikia hazma hii ni uendelezaji na uimarishaji wa ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa na hivyo kufungia fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji,” amrsema Rais Samia.
Hata hivyo amewataka wafanyabiashara kutumia maenesho hayo kukuza biashara zao na kuzitumia taasisi za serikali kufanikisha azma hiyo ya kufanya biashara kwenye nchi za nje hasa eneo huru la biashara Afrika (AfCFTA).
“Wafanyabishara kutoka Tanzania kupitia maonesho haya jifunzeni kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nje ili muweze kukuza biashara zenu, itumieni Tantrade kufanikisha biashara zenu kwa kutazama fursa zilizopo kwenye masoko ya kimataifa,” amesema
Amesema Mwaka 2023 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilisajili miradi 504 yenye thamani ya dola za Marekani Bilioni 5.68 hii ni kwa sababu watu wanakuja Tanzania wanaona maonesho hayo na kuvutiwa kuwekeza.
Naye Rais wa Msumbiji, Filipe Nyuse akifungua maobesho hayo amesema kuwa anaishukuru serikali ya Tanzania kwa kuisaidia nchi yake katika kupambana na suala la ugaidi ambalo amelitaka kuwa lilikuwa linazorotesha uchumi wa nchi hiyo.
Rais Nyusi amesema Tanzania imesimama pamoja na watu wa Msumbiji kipindi chote mpaka sasa hali katika nchi hiyo imetulia.
Amesema utulivu na amani ni muhimu kwa matumizi ya fursa za nishati kati ya nchi hizo mbili zenye akiba kubwa ya gesi asilia katika mkoa wa Mtwara na jimbo la Delgabo Msumbiji.
Aidha amesema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ambayo ni kati ya mwaka 2018 na 2023 jumla ya biashara za nje za nchi hizo mbili katika uagizaji na mauzo ya nje yalifikia dola za Marekani Milioni 250 tu.