Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua mfumo mpya wa Sera ya elimu huku akiweka msisitizo wa Serikali kupitia upya maslahi ya kada ya ualimu nchini.
Amesema dhamira ya mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ni kumuandaa kijana anayejiamini na mwenye nyenzo stahiki za kukabiliana na ushindani wa kikanda na kimataifa ili aweze kutumia na kunufaika na utajiri wa rasilimali zilizopo nchini.
Rais Samia ameyasema hayo leo Februari 1, 2025 jijini Dodoma wakati akizindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 – Toleo la 2023 ambapo ameeleza kuwa uwepo wa Sera hiyo utasaidia kuleta matokeo ya elimu yanayotakiwa .
Aidha ameitaka Wizara ya Fedha, Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na TAMISEMI kuwezesha na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera na mitaala mipya ili ilete matokeo yaliyokusudiwa”, amesema Rais Samia.
“Katika maboresho yatakayofanywa, Walimu lazima wazingatiwe na sisi kama Serikali tutaendelea kuajiri Walimu wenye sifa na kuwapa mafunzo stakihi ili waweze kuendana na mwelekeo wa sera hiyo,serikali itapitia upya maslahi ya kada ya Ualimu nchini.
Ameeleza kuwa, Sera na mitaala imewekewa msisitizo wa elimu ujuzi na ufundishwaji wa somo la ujasiriamali ambalo litamuwezesha kijana kupata misingi ya biashara na kutoa mchango kwa taifa, pia Sera ina lengo la kutambua na kurasimisha ujuzi na stadi
“Kwa muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuongeza Pato la Taifa hadi kufikia Dola bilioni 700, ni wazi kwamba Sera hii itakuwa nyenzo muhimu kwa kuongeza wigo wa watenda kazi wenye ujuzi watakaoshiriki kujenga uchumi wa nchi,” amesema Rais Samia.
Amesema ili kumuandaa kijana kushindana kikanda na kimataifa, sera hiyo pia itawasaidia wanafunzi kupata elimu ya lugha mbalimbali za kimataifa mbali na kiingereza ikiwemo; kichina, kifaransa na kiarabu kwani ndizo lugha zinazoendesha uchumi duniani.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa Sera ya Elimu ni kanuni ambazo zinaongoza nchi kuweza kufikia maamuzi kuhusu maendeleo ya elimu na kufikia malengo ya nchi pia, ndiyo mwongozo wa kuandaa mtaala wa elimu unaotumika kufundishia wanafunzi.
“Sera hii mpya itatuwezesha kubadili mfumo wetu wa elimu ili kuweza kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi wa kumudu mabadiliko ya teknolojia”, amesema Mhe. Dkt. Mpango.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa chimbuko la mabadiliko hayo ya kihistoria ni maono yako Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwani mabadiliko mengi yanayotokea kwenye serikali huwa yanaanza kwa wataalam, Waziri husika na Rais anatoa maelekezo lakini kwenye mabadiliko haya alianza Rais, yakaja kwa Waziri husika na wataalam wakaja kutekeleza maono yake.