Katika kukuza soko la nyama hapa nchini Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema inadhamira ya kufanya kampeni ya kuchanja mifugo kwa kufuata kalenda ili kuongeza soko la nyama nje ya nchi kutoka tani 12 ya sasa hadi tani 100.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) Mjini Morogoro wakati akifungua maadhimisho ya wiki ya kumbukizi ya 18 ya Hayati Edward Moringe Sokoine yanayo fanyika Kampasi Kuu ya Edward Moringe Sokoine .
Amesema licha ya wafugaji kuchanja mifugo yao, bado zoezi hilo haliratibiwi ipasavyo hivyo kufanya baadhi ya nchi kushindwa kununua nyama hapa nchini kwa sababu ya kutochanja mifugo.
“Wachina wanataka nyama yetu, lakini wanaiogopa, wanasema inamaradhi, kwa sababu hatuchanji, si kweli, kwamba watu hawachanji kabisa, yawezekana watu wanachanja kule kwenye Halmashauri, lakini hakuna utaratibu wenye kueleweka.” alisema Waziri Ulega.
Pia Waziri Ulega amesema,kuanzishwa kwa kampeni hiyo kutatoa fursa kwa wanafunzi wanaosoma Shahada za Mifugo ikiwemo wanaotoka SUA kujifunza kwa vitendo na kwamba kutaongeza ajira kwa vijana wengi wanaomaliza Elimu ya Juu hapa nchini.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda, amesema katika kumuenzi Hayati Edward Moringe Sokoine, SUA kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi, wapo katika hatua za mwisho za kuandika kitabua, cha kumbukumbu ya Hayati Sokoine.
“Chuo chetu kwa kushirikina na Taasisi ya Uongozi tupo katika hatua za mwisho za kukamirisha uandishi wa kitabu hicho, kwahiyo kitakapokuwa tayari, tumekubaliana na wenzetu wa uongozi, tutalifanya liwe tukio kubwa la uzinduzi wa hicho kitabu.” amesema Prof. Chibunda.
Amesema kwa mwaka huu 2023 SUA itaadhimisha kumbukizi ya Sokoine kuanzia Mei 23 hadi 26 kwa kufanya shughuli mbalimbali kama kufanya mkutano wa Kisayansi kwaajili ya wanataaluma, watafiti, wanafunzi na wadau.
Kwa mwaka 2023 maadhimisho hayo yanabebwa na Kauli mbiu isemayo, Mazingira wezeshi kwa vijana kushiriki katika Kilimo, sera , miongozo na utendaji, ambapo kauli hiyo inalenga kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuwawekea mazingira rafiki.