Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Ruvuma
Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ina mpango kabambe wa kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi ambao wamekuwa na uhitaji wa umeme kwa muda mrefu hivyo katika Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ambako kuna majimbo mawili yenye jumla ya vijiji 169 tayari vijiji 100 vimeshapatiwa huduma ya umeme kupitia mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili.
Hayo yamesemwa jana na mhandisi Evans Kabingo wakati akitoa mada kwenye warsha ya Baraza la Jumuia za Vijana na Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyofanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wananchi kilichopo mjini Mbinga ambacho pia kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali akiwemo Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga.
Amesema kuwa idadi ya vijiji vitakavyonufaika na umeme katika Jimbo la Mbinga mjini ni vijiji 26 na Jimbo la Mbinga vijijini vijiji 74 ambavyo hufanya jumla ya vijiji 100 na kwamba kwa jimbo la Mbinga mjini mradi huo wa REA utagharimu kiasi cha sh. Bilioni 9.08 na Jimbo la Mbinga vijijini itagharimu kiasi cha sh. bilioni 19.81.
‘Mradi huu unatekelezwa na Kampuni ya Namis Corporate Limited ya kutoka nchini Tanzania na katika majimbo hayo mawili tayari mkandarasi amekamilisha kuwasha umeme vijiji 41 kati ya 100 na bado anaendela na utekelezaji wa kuwasha vijiji 59 pamoja na kazi za nyongeza ya kilimeta 2 za msongo mdogo wa mtambo wa REA.”amesema Mhandisi Kabingo.
Hata hivyo amesema kuwa kazi bado inaendelea ya kusambaza huduma ya umeme vijijini hivyo amewataka wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali kwani Wakala wa Umeme Vijijini (REA) bado wanafanya kazi ya kuhakikisha wananchi wote hapa nchini hasa waliopo vijijini wanapata umeme na si vingininevyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amewaasa wananchi ambao bado huduma ya umeme haijawafikia kuendelea kuwa wavumilivu na kwamba Serikali imekwisha toa fedha kwa ajili kumalizia vijiji vyote vilivyobaki ili viweze kuwa na umeme ambao utawapatia fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo kufungua viwanda vidogo vidogo vya kuchakata nafaka, saluni, uselemala na ufundi pamoja na wajasiliamali kuwa na majokofu kwa ajili ya kuweka vinywaji baridi na moto.
Hata hivyo amemuhimiza Mkandalasi Namis Corporate Limited kuharakisha mradi huo wa REA kwenye maeneo yaliyobaki vijijini kwani wananchi wana haki ya kupata huduma ya umeme kama ilivyo maeneo mengine ya vijiji yaliyopatiwa umeme na hata kubaliana kuona mradi huo unasuasua kwa vijiji vilivyobaki .
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Namis Corporate Limited Mhandisi Shaidu Rutakolezibwa amesema kuwa hadi kufikia Desemba mwaka huu vijiji vyote vilivyosalia atakuwa amekamilisha na kwamba kwa wilaya nzima umeme utakuwa umewaka licha ya kuwa alikuwa na matatizo madogo madogo ambayo tayari yameanza kufanyiwa kazi .