Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)  ipo katika hatua mbalimbali za kujenga mizani mpya katika mtandao wa barabara kuu nchini ili kudhibiti uharibifu wa barabara unaosababishwa na uzidishaji uzito wa magari.

 Hayo yameelezwa leo Mei 22, 2023  bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara yake kwa Mwaka 2023/24.

“Mizani hiyo ni pamoja na mizani ya Rubana mkoani Mara ambapo ujenzi wa barabara za maingilio, majengo ya Ofisi na eneo la mizani unaendelea, mizani ya Matundasi katika barabara ya Chunya – Makongorosi mkoani Mbeya, mizani ya Bulamba katika barabara ya Bulamba – Kisorya mkoani Mara”, alieeleza Prof. Mbawara.

Alitaja mizani mingine kuwa ni ya Igagala katika barabara ya Njombe – Moronga – Makete mkoani Njombe, mizani ya Mingoyo ya upande wa pili mkoani Lindi itakayopima uzito wa magari yanayotoka mikoa ya Ruvuma na Mtwara, mizani ya Mdori mkoani Manyara ambayo itapima uzito wa magari yanayotoka Singida na Dodoma na mizani ya Kizengi mkoani Tabora.