Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akieleza jambo wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi iliyofanyika kwenye viwanja vya Tumbaku, Mkoani Morogoro.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Bw. Tumaini Nyamhokya (kulia) akieleza jambo wakati wa hafla hiyo
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu akieleza jambo wakati wa hafla hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akitoa tuzo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (kushoto) wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi kwenye viwanja vya Tumbaku, Mkoani Morogoro.
……………………………….
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kusimamia masuala ya usalama na afya mahala pa kazi kwa kuwa ni haki ya msingi wa kila mfanyakazi nchini.
Prof. Ndalichako ameyasema hayo Aprili 28, 2023 katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi kwenye viwanja vya Tumbaku, mkoani Morogoro.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Mazingira salama na yenye afya kazini ni kanuni na haki ya msingi mahali pa kazi.”
Amesema Rais Samia amekuwa kinara katika kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inalindwa kwa kuendelea kuimarisha Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA).
Waziri Ndalichako amewataka OSHA kuendelea kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi na kuwahamasisha waajiri kuweka mifumo sahihi ya usalama na afya katika maeneo yao ya kazi na kuendelea kuzingatia sheria na kanuni za usalama na afya sehemu za kazi.
Akizungumza awali, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema kuwa masuala ya usalama na afya ni mtambuka na yanagusa nyanja zote za kiuchumi, hivyo OSHA imejipanga katika kuhakikisha mfanyakazi nchini wanafanya kazi kwenye mazingira yenye usalama na afya.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba ameeleza kuwa ili mwajiri awe na tija na ufanisi katika mazingira yake ya kazi ni lazima azingatie usalama na afya wa wafanyakazi wake.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amesema Serikali, Waajiri na Wafanyakazi wanawajibu wa kuhakikisha sehemu za kazi wakati wote zinakuwa salama.