Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ruvuma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama (MB) wa Peramiho amesema Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Songea imedhamiria kufungua shamba kubwa la miwa na kiwanda cha kuzalisha sukari katika kijiji cha Muhukuru.
Kauli hiyo imetolewa mkoani Ruvuma katika Kijiji cha Lupokela leo tarehe 30/09/2023 katika Maadhimisho ya siku ya Kahawa yaliyoandaliwa na Kampuni ya Aviv wawekezaji wa mashamba ya Kahawa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
“Tunaamini tukifungua shamba lingine Muhukuru tunaweza kuzalisha ajira nyingine nyingi na kuongeza mapato ya Halmashauri na pato kwa wananchi.” amesisitiza.
Wawekezaji kampuni ya Aviv wanazalisha asilimia 4.5 ya kahawa yote inayozalishwa nchini ambayo inauzwa nje ya nchini, na wanasaidia nchi kupata fedha za kigeni, ambazo zinawezesha serikali kujenga miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Aidha Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuweka mkazo katika kufungua kilimo ili kusaidia kuchochea uchumi na kutoa ajira ili kuhakikisha kilimo kinakuwa na faida katika kufungua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
“Wananchi ni mashuhuda wa uwekezaji uliofanywa na Kampuni ya Aviv katika kilimo cha kahawa; ulivyowezesha kufanya mabadiliko ya kijamii, uchumi na mabadiliko ya mwenendo wa maisha ya wananchi katika vijiji vinavyozunguka mradi,” amefafanua.
Ameongeza kusema mwekezaj Kampuni ya Aviv anashiriki katika ujenzi wa miradi mingi katika vijiji vinavyozunguka mradi kama utaratibu wa serikali unavyoelekeza kwa wawekezaji, kwamba washirikiane na wananchi katika kurudisha mchango wa kile walichokivuna kama faida. Amewaomba wananchi kutobweteka na badala yake kuendelea kujitoa katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Meneja wa Shamba la Kampuni ya Aviv Tanzania Bw, Hamza Kassim amesema siku ya leo tunadhimisha siku ya kahawa duniani, maadhimisho ambayo yanayofanyika kila tarehe 01 ya mwezi wa 10, kila mwaka.
Ameongeza kusema, kampuni ya Aviv wamefanikiwa kuwa na uzalishaji endelevu kwa sababu ya kujenga miundo mbinu ya Umwagiliaji ambayo imeleta tija katika kuchangia miradi mabalimbali ya maendeleo kwa jamii.
“Kampuni ya Aviv; inaendelea kujenga uwezo kwa wananchi ili waweze kuwa wakukulima wa kilimo cha kahawa chenye tija Zaidi,” amefafanua.
Awali Rose Choma Mkulima amesema mradi wa kampuni ya Aviv wamesaidia wakulima katika kuwapa wananchi mbegu zenye ubora na kutoa ajira kwa wazawa ambazo zimesaidia kuinua pato kwa wananchi.