Serikali inakusudia kufufua Shirika la Taifa la Uwakala wa Meli (NASACO), katika jitihada za kuboresha huduma katika Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia wateja wake kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza na wahariri, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedith Kakoko, amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuanzisha chombo hicho kitakachohusika na uratibu wa meli zinazoingia Bandari ya Dar es Salaam na nyingine.

“Tumekuwa na baadhi ya mawakala (clearing and forwarding agents)  ambao si waaminifu. Katika ziara zangu za kuzungumza na watumiaji wa Bandari yetu ya Dar es Salaam, nimelalamikiwa sana kuhusu mawakala. Sasa dawa yao inakuja,” anasema Kakoko.

Anasema, zamani kazi hizo za uwakala zilifanywa na NASACO huku ikiwa na ufanisi mkubwa katika shughuli zake, lakini baadaye kwa maslahi ya wachache ikasambaratishwa, hivyo sasa Serikali inaandaa utaratibu wa kuirejesha kampuni hiyo kwa maslahi mapana ya nchi.

“Tunaangalia uwezekano wa kufufua NASACO mpya… lazima tuwadhibiti hao wanaotuharibia biashara yetu, hata awe tajiri kiasi gani, unakaa na gari muda mrefu ili kupata storage,” anasema Kakoko.

Katika kuanzishwa kwa chombo hicho na hatima ya kampuni za uwakala wa meli, Mhandisi Kakoko anasema mawakala hao wajipange kufanya kazi kupitia chombo hicho kitakachoanzishwa, kwani ndicho kitakachokuwa kiunganishi muhimu.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari anasema Serikali imewapatia lengo la kukusanya Sh trilioni 1 katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Anasema agizo hilo limetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa. Katika mwaka wa fedha wa 2015/16 Bandari walikusanya Sh bilioni 662, huku lengo likiwa ni kukusanya Sh bilioni 631.

“Tunaamini kwa kutekeleza miradi iliyopo, kubana matumizi, kuziba mianya ya upotevu wa mapato, kuongeza ufanisi na jitihada za kutafuta masoko, lengo letu la kukusanya Sh trilioni 1 kwa mwaka litafikiwa,” anasema Kakoko.

Mhandisi Kakoko anasema sambamba na agizo hilo, Prof. Mbarawa ameagiza Mamlaka hiyo kuchunguza chanzo cha kupungua kwa shehena ya mizigo na kuchukua hatua stahiki za kuhakikisha mizigo inaongezeka.

Anasema, katika kutekeleza agizo la waziri, tayari uongozi umeanza kuchukua hatua za kuhakikisha kampeni ya kutafuta masoko inaendeshwa ipasavyo.

“Matumizi yetu yameshuka. Baada ya kutoa kodi za Serikali, ambazo kwa mwezi ni wastani wa Sh bilioni 3, mrabaha zaidi ya Sh bilioni 93 tulizolipa kwa Msajili wa Hazina, tumebakiwa na kiasi cha Sh bilioni 128. Tumeruhusiwa kuingiza fedha hizo kwenye miradi,” anasema Kakoko.

Mhandisi Kakoko anasema, maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam yamepangwa katika mpango utakaogharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 690 kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na fedha za ruzuku kutoka Trade Mark East Africa na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID).

Anasema, Benki ya Dunia kupitia mfuko wa International Bank for Reconstruction and Development (IBRD), itatoa mkopo wa masharti nafuu wa kiasi cha dola za Marekani milioni 600. DFID watatoa ruzuku ya kiasi cha dola za Marekani milioni 30 na Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari itachangia kiasi cha dola za Marekani milioni 60.

Anayataja maeneo yatakayofaidika na mpango huo kuwa ni uboreshaji na uongezaji wa kina kufikia mita 14 katika gati namba 1 hadi 7 ili kuwezesha meli kubwa kutia nanga, uboreshaji na uongezaji wa kina kufikia mita 14 katika gati namba 8 hadi 11 zilizokodishwa kwa TICTS ili kuwezesha meli kubwa kutia nanga.

Miradi mingine ni ujenzi wa gati mpya ya kushushia magari katika eneo la Gerezani Creek, uchimbaji kuongeza kina cha lango la kuingilia meli hadi mita 14 pamoja na sehemu ya kugeuzia meli na kupanua lango la kuingia bandarini, ufungaji wa conveyor system na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia nafaka.

Anazitaja sehemu nyingine zitakazoguswa na mpango huo kuwa ni ujenzi wa gati mpya namba 13 na 14, kuhamisha gati la mafuta la Kurasini (KOJ) pamoja na kuhamisha mabomba ya mafuta katika eneo la KOJ, kujenga na kuboresha mtandao wa reli ndani ya bandari na ujenzi wa sehemu ya kupakilia na kushushia mizigo kwenye mabehewa, na kukamilisha ujenzi wa jengo la ‘One-Stop Centre’ Barabara ya Sokoine.

Anasema mpango huo unaolenga kuboresha mifumo yote bandarini, utahusisha kuboresha na kupanua barabara ya Bandari na Mivinjeni kupunguza msongamano wa magari yanayoingia na kutoka bandarini. Kuboresha mifumo ya Tehama kuongeza ufanisi na kurahisisha kazi ya kupakia na kupakua mizigo.

Kakoko anasema bandari inatumia mfumo wa E-Payment kwa ajili ya malipo, ambao utaunganishwa na mifumo mingine ya kisasa ya Tehama ya Enterprise Resource Planning (ERP) na Terminal Operating System (TOS).

Anasema Bandari ya Dar es Salaam inazo Scanner 3 na TPA inategemea kuongeza nyingine 2, kwa ufadhili wa Trade Mark East Africa (TMEA), ambazo zitatosheleza mahitaji ya sasa. Mamlaka inakamilisha mradi mkubwa wa ulinzi ambao utahusisha, kusimika mifumo ya ulinzi katika geti Na. 2, 3, 7, 8, KOJ, Dock yard, na makao makuu.

Mradi huo utakwenda sambamba na kusimika kamera za ulinzi katika Bandari ya Dar es Salaam na makao makuu, kujenga uzio wa umeme, kusimika vipaza sauti katika Bandari ya Dar es Salaam na makao makuu pamoja na kuweka mifumo ya ulinzi kwenye mageti mengine.

Akizungumzia kushuka kwa mizigo bandarini, Mhandisi Kakoko anasema, mwezi Juni, mwaka huu  shehena ilishuka kwa kiwango cha tani milioni moja. Lakini anasema jitihada zimeanza kufanyika kuwarudisha wateja ambao waliamua kuacha kutumia Bandari ya Dar es Salaam.

“Nilikuwa Rwanda hivi karibuni katika maonesho yao ya biashara, nilikutana na wasafirishaji ambao wamekuwa wakitumia bandari yetu, wakanielezea changamoto kama 11, nikasuluhisha 3 palepale…tumefungua ofisi pale Kigali ili kushughulikia soko la Rwanda,” anasema Kakoko.

Kuhusu shehena ya Zambia kupungua, anasema baadhi ya wafanyabiashara waliamua kuhamia katika Bandari ya Durban, Afrika Kusini, ambako kuna umbali wa zaidi ya kilomita 4,000 ikilinganishwa na umbali kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kutokana na huduma zisizoridhisha.

Lakini anataja sababu nyingine iliyochangia kushuka kwa shehena kutoka nchini Zambia kuwa ni kitendo cha China kupunguza kiwango cha kuagiza shaba kutoka nchini humo na ongezeko la tozo.

Hata hivyo, kwa ujumla wake katika biashara ya Bandari, kila inapofika mwezi Julai na Agosti, mizigo hupungua bandarini na huanza kufurika tena inapofika Septemba, Oktoba, Novemba na Desemba kwa ajili ya bidhaa za matumizi ya sikukuu.