Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali imesema itaendelea kujenga uelewa kwa wadau mbalimbali kuhusu Kanuni na Miongozo inayosimamia Biashara ya Kaboni.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne (Mei 21, 2024) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt Selemani Jafo wakati wa semina kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira pamoja na Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Biashara ya Kaboni.
Dkt. Jafo amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko tabianchi ikiwemo uratibu wa biashara ya kaboni ambayo inalenga kupunguza uzalishaji wa gesi joto duniani.
Ameongeza kuwa changamoto hizo za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zimeibua fursa ambazo zimesaidia uhifadhi endelevu wa mazingira na mwaka 2022 Serikali iliandaa Kanuni kwa ajili ya kuratibu biashara hiyo kwa kampuni, taasisi na watu binafsi.
“Malengo makuu ya Kanuni na Mwongozo ni kuweka utaratibu na masharti ambayo wadau watapaswa kuzingatia wakati wa utekelezaji wa miradi mipya na miradi inayoendelea ili kuweka mazingira rafiki ya usimamizi wa biashara hii,” amesema Dkt. Jafo.
Ameongeza kuwa malengo ya Serikali ni kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi kwa wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi, wawekezaji na wananchi kujitokeza kusajili miradi ya biashara ya kaboni ambayo inaratibiwa na Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kilichopo mkoani Morogoro.
Pia, Mhe. Dkt. Jafo ameeleza kuwa kutokana na wawekezaji wengi kuanza kujitokeza na kusajili miradi, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma kwa makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo Wabunge na makundi mbalimbali ya kijamii ili kuhakikisha Kanuni na Miongozo ya biashara hiyo inafahamika vyema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga ametoa rai kwa Serikali kuandaa mpango wa kutangaza fursa za biashara ya kaboni ikiwemo kuanzisha kitengo maalum cha masoko ambacho kitatangaza fursa za biashara hiyo kupitia mikutano, makongamano na warsha nje ya nchi.
“Tulikuwa katika mkutano fulani nje ya nchi niliona mataifa yetu ya nchi jirani yakitumia fursa za kutangaza biashara ya kaboni katika mkutano ule ….na sisi hatuna budi kujipanga ili kutangaza biashara hii,” amesema Mhe. Kiswaga ambaye pia ni Mbunge wa Kalenga.
Akichangia mada katika semina hiyo, Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Riziki Lulida ameiomba Serikali kuhakikisha inafanya tathmini ya ukaguzi wa misitu mbalimbali nchini ambayo kwa sasa imevamiwa na makundi mbalimbali ya wafugaji na wakulima hatua itakayosaidia kutunza na kuhifadhi mazingira ya maeneo hayo.
Mada ya biashara ya kaboni katika semina hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa NCMC Prof. Eliakim Zahabu.