Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali imeahidi kutatua changamoto zinazozikabili Taasisi za dini nchini huku ikilenga kuboresha mazingira ya kiutendaji na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vya ubora.

Ahadi hii inahusisha hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na urahisishaji wa taratibu za usajili na usimamizi wa huduma za kijamii zinazotolewa na taasisi hizo jambo ambalo litasaidia kuongeza ufanisi wa taasisi hizo katika kutekeleza majukumu yao ya kijamii na kiroho.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 15,2024 Jijini Dodoma na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ally Mwinyi wakati akizungumza kwenye Mkutano wa nane wa Baraza Kuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) 2024 na kueleza kuwa Serikali zote mbili zitaendelea kusimamia misingi hiyo kwa manufaa ya Watanzania.

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zote kwa ujumla wake zinazingatia haki na Uhuru wa kuabudu kama msingi muhimu wa kuleta umoja kwa Watanzania na kudumisha Amani.

“Uhuru wa kuabudu ni haki ya msingi inayohakikisha kwamba kila mtu katika jamii ana haki ya kuchagua, kuanzisha, na kuendeleza imani ya kidini anavyotaka,haki hii inajumuisha uhuru wa Kujiunga na Dini,kubadili dini, au kutokuwa na dini kabisa bila hofu ya unyanyasaji au kulazimishwa,”amesema.

Amesema, “napenda nikuhakikishie kuwa Serikali zetu zote mbili zinazingatia haki na uhuru wa kuabudu kama msingi muhimu wa kuleta umoja wa Watanzania na kudumisha Amani”.

Pamoja na hayo amemuahidi Baba Askofu wa Kanisa hilo kuwa Serikali itaendelea kutambua mchango wa Tasisi za kidini kwenye jamii na kuthamini kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Taasisi za hizo katika kuhubiri amani na kuhudumia jamii .

“Kwa kutambua umuhimu huu Serikali na taasisi nyingine zinahitajika kulinda haki hii dhidi ya ukandamizaji, ubaguzi, na vitendo vya vurugu vinavyoweza kuathiri Taasisi za dini, tunatambua mchango wa Taasisi za dini kwa watanzania hususani katika sekta za Afya,Elimu,Maji safi na Kugusa watu wenye mahitaji maalum wakiwemo walemavu na Wazee hivyo hatuna budi kuwapa moyo na kuwasihi muendelee kuwasaidia wananchi kwa kushirikiana na Serikali, “amesisitiza.

Aidha ameaahidi kwamba ,” Tutaendelea kuwapa ushirikiano katika kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazozikabili Taasisi za dini ili ziweze kutekeleza majukamu yao kwa ufanisi zaidi, niwatoe hofu kwa sababu Serikali inatambua umuhimu wa umoja, kwahivyo tutaendelea kuchukua kila hatua kuhakikisha tunalinda na kudumisha umoja wa Watanzania na kuhakikisha wananchi wote wanaishi kwa kushirikiana na kuheshimiana”amesema

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa hilo la TAG Dkt Barbanas Mtokambali ametumia fursa hii kumpongeza Dkt Mwinyi na Serikali ya Mapinduzi kwa kuonesha msimamo madhubiti kwa vitendo wenye kuleta usawa wa haki ya kikatiba katika uhuru wa kuabudu .

Hatua ni pale Dk. Mwinyi alipo laani vitendo vya unyanyasaji katika maeneo mbalimbali huko Zanzibar dhidi ya watu wa imani tofauti pamoja kuhimiza hali ya kuvumiliana na kustahimiliana katika taratibu za ibada za imani za katika made madhehebu ya dini tofauti ila mradi pasivunjwe sheria.

“Tunakupongeza sana wewe Raisi Mwinyi na Serikali ha Mapinduzi kwa kuonesha msimamo madhubuti wenye kuleta usawa na haki ya kikatiba katika uhuru wa kuabudu pale ulipo laani vitendo vya unyanyasaji katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar dhidi ya watu wa imani tofauti pamoja na kuhimiza hali ya kuvumiliana na kustahimiliana katika taratibu za ibada za imani za kidini katika madhehebu ya dini tofauti ili mradi pasivunjwe Sheria, “amesema na kuongeza;

“Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Serikali kwa vyombo vya habari,Walaka wa SMZ tarehe 30 March 2024 kuhusu uvumilivu wa kidini,inawezekana tunapoongea uvumilivu wa kidini duniani basi Zanzibar mpo juu sana na Ikumbukwe kuwa hata ukristu wakati umeingia ukanda huu wa Afrika Mashariki ulipitia Zanzibar dio maana bado kuna mabaki ya majenjo ya kale yaliyotumika kama Makanisa”, amesema.

Please follow and like us:
Pin Share