Na Happiness Shayo, JamhuriMedia, Njombe

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa Sekta ya Misitu ili kuleta ufanisi na manufaa zaidi katika kuchangia ukuaji wa pato la Taifa (GDP) na kunufaisha wananchi kupitia rasilimali za misitu zilizopo hapa nchini.

Ameyasema hayo leo Machi 22, 2025 Mkoani Njombe wakati wa kikao kazi kilichoshirikisha viongozi wa wizara, taasisi na wadau wa sekta ya misitu na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu misitu kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa haraka.

“Sisi kama Serikali tunajivunia Jukwaa hili kwa kuwa kupitia vikao vyake masuala mengi na ya msingi yamepatiwa ufumbuzi. Kwa masuala ambayo pengine nyie wadau mnaona kuwa bado yana ukakasi, naomba kuwahakikishia kuwa Wizara yangu inaendelea kutafuta ufumbuzi wake” amesema Waziri Chana

Waziri Chana amesisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wa sekta hiyo ili kuwasaidia katika kufanya biashara za mazao ya misitu kwa ufanisi huku akiweka mkazo juu ya kupitia na kufanya maboresho kwenye Sheria na Kanuni zilizopo ili kuendana na matakwa ya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 kama ilivyotekelezwa hivi karibuni.

“Tumefanikiwa kufanya mapitio na kuboresha kanuni zinazosimamia utaratibu wa usafirishaji wa Venia kwenda nje ya nchi kwa TSN 807 la mwaka 2024; kanuni za udhibiti na usimamizi wa matumizi ya msumeno wa moto zilizotangazwa kwa Tangazo la Serikali Na 62 la mwaka 2025; kanuni za mazao na Huduma za Misitu kupitia TSN. 132 la mwaka 2025.”amesema Waziri Chana.

Aidha, Waziri Chana ametolea ufafanuzi juu ya kanuni za jumla za ufugaji Nyuki zilizotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Namba 131 la mwaka 2025 na marekebisho ya kanuni ya uzalishaji, usafirishaji na uuzaji wa mkaa mbadala zilizotangazwa kwa Tangazo la Serikali Na. 85 la mwaka 2024.

Katika hatua nyingine Waziri Chana amewahimiza wadau hao kujikita katika kuongeza thamani ya mazao ya misitu iliyopo hapa nchini ili kuwa na bidhaa zenye thamani ya juu zinazozalishwa hapa nchini, kuongeza ajira, kuongeza kipato kwa wananchi, wawekezaji na Taifa kwa ujumla kupitia mnyororo wa thamani wa biashara hiyo.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na Katibu wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Naibu Katibu Mkuu, CP Benedict Wakulyamba, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Deusdedith Bwoyo Kamishna wa uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wadau na wafanyabiashara wa mazao ya misitu, wakuu wa Taasisi za Wizara kutoka TaFF, TAFORI,TFS na vyuo vya mafunzo, maafisa Waandamizi wa Idara ya Misitu na Nyuki, makamanda wa TFS na wadau wengine ikiwa ni siku moja baada ya Wizara hiyo kuadhimisha siku ya Misitu Duniani na Upandaji miti kitaifa iliyobebwa na kaulimbiu “Ongeza thamani ya mazao ya misitu kwa uendelevu wa rasilimali kwa kizazi hiki na kijacho.”