Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
SERIKALI imesema ipo tayari kusikiliza maoni ya kila mmoja ili kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inakuwa halisi na shirikishi.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, wakati akifungua mkutano wa asasi za kiraia (Azaki) kuhakiki Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema maoni ya wananchi na wadau mbalimbali ni muhimu katika uandaaji kwani ndio msingi wa kuandaa Dira hiyo.
“Tunawahakikishia tutashirikiana katika kuandaa dira hii muhimu pamoja na kuwepo na majadiliano ya pamoja baina ya Serikali na wadau wa maendeleo badala ya ukosoaji ili kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ,” amesema.
Aidha amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu wake wa kutaka maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ishirikishe wananchi wote akiwapongeza Watanzania kwa kushiriki kikamilifu kwenye uandishi wake.
Amesema suala la dira lilianza zamani tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere aliyetangaza maadui wa Taifa ambao ni umaskini, ujinga na malazi kabla ya kuja na Azimio la Arusha ambalo lilikuja na mikakati ya kupambana na maadui hao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge ameainisha kuwa kukuza uchumi shindani ndani ya mikoa ni njia muhimu ya kufanikisha maendeleo endelevu, akitolea mfano wa nchi ya Kenya ambako kaunti zinashindana kwa vigezo vya kuzalisha ajira na kujumuisha makundi ya pembezoni.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa kuwajumuisha wadau wa kiraia katika uandishi wa Dira ya Maendeleo ya taifa ya mwaka 2050.
Naye Lucas Kifyasi, Mkuu wa Programu za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, ameongeza kuwa utekelezaji wa dira hiyo utahitaji kipaumbele katika elimu, hasa kwa kuzingatia mapinduzi ya viwanda yanayotarajiwa kuimarika miaka 25 ijayo.
Amesisitiza kuwa elimu na teknolojia ni nguzo muhimu za maendeleo endelevu.
Mkutano huo umeonyesha dhamira ya pamoja kati ya serikali, AZAKI, na wadau wa mbalimbali katika kuhakikisha Tanzania inafanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.