N Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
SERIKALI imesema itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wazabuni wa ndani kwa lengo la kujifunza na kuona changamoto mbalimbali walizonazo na kisha kuzifanyia kazi.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya wakati akifungua semina iliyoandaliwa na Benki ya Duniani kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) ikilenga kuwajengea uelewa na kusikiliza changamoto zao.
Amesema wazabuni wa ndani ya nchi wanapaswa kujengewa uwezo ili kuweza kuongeza katika kupata fursa kupamoja na kuongeza fursa za ajira.
Amesema katika kutimiza mikakati hiyo mwaka 2023 Serikali baada ya kupata kibali cha Bunge iliweza kufanya maboresho na kuanzisha sheria mpya ya ununuzi wa umma ambayo imetoa fursa zaidi kwa watanzania.
”Sheria hii ipo kwaajili ya kutafsiri maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Lakini katika kazi ambazo zitazidi kiwango Sh. Bilioni 50, kampuni za Tanzania zinauwezo wa kufanya kazi hizo kwa mashirikiano na kampuni za nje.
”Pia tumekwenda mbali zaidi kutasfiri namna wanavyoweka upendeleo kwa watanzania hasa kwenye maeneo yanayotumia rasilimali au malighafi nchini na yale yanayoajiri watanzania kuna upendeleo wao,” alisisitiza.
Aidha alisema katika kutekeleza bajeti ya serikali,asilimia kadhaa inayotoka katika bajeti ya serikali inakwenda kwenye ununuzi na ugavi wa umma ambapo kiwango hiki kinapita mikono ya wazabuni na wakandarasi.
”Katika kutekeleza bajeti hiyo tunashirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo benki ya dunia katika kuhakikisha miradi inayofadhiliwa na benki hiyo ya dunia inahakikisha ushiriki wa watanzania inakwenda zaidi katika eneo hilo ili kuhakikisha malengo yanafikiwa ipasavyo,” amesema.
Kwa Upande wake Kamishna anayesimamia Maendeleo ya Sera za Ununuzi wa Umma na Ugavi kutoka Wizara ya Fedha, Fredrick Mwakibinga amesema mkutano huo ni wa kuwakutanisha wakandarasi na wazabuni kutoka kampuni mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kampuni za kitanzania zinapata tenda katika miradi inayofadhiliwa na Benki ya dunia pamoja na washirika wengine wa kimaendeleo.
Amesema mkutano huo umegusa maeneo mbalimbali ya majadiliano ikiwemo namna ya kupata fursa ya kupata miradi hiyo, changamoto wanazokabiliana nazo wakandarasi pamoja na kuona namna ya zabuni zinavyogawanyishwa kwa wakandarasi wazawa na wa nje.
Kwa upande wake, Meneja Uendeshaji, wa Benki ya duniani nchini, Milena Stefanova amesema miradi yao inakuwa na masharti kwa sababu wanataka ijengwe kwa kuzingatia sifa na vigezo.