NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amesema serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kuiba mali baada ya ajali kutokea.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Makete, Festo Sanga (CCM) aliyeuliza swali kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Chumbuni, Ussi Salum Pondeza (CCM), Sanga alitaka kujua mkakati wa Serikali wa kuchukua hatua kali zaidi kwa watakaokutwa wanachukua mafuta baada ya ajali kutokea kutokana na matukio hayo kujirudia moja kwa moja.
Katika swali la msingi, Pondeza ametaka kujua serikali ina chukua hatua gani kwa wananchi wanaochukua mafuta baada ya magari ya kubeba mafuta kupata ajali.
Akijibu swali hilo, Sillo amesema kwa mujibu wa Sheria ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022 kifungu cha 258 na 265 ni kosa kisheria kuchukua mali ya mtu mwingine bila idhini ya mwenye mali ama kuwa na dai la haki.
Amesema kitendo cha kuchukua mafuta baada ya magari ya kubeba mafuta kupata ajali na bila kuruhusiwa na mwenye mali ni kutenda kosa la wizi.
Sillo amesema Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kuwachukulia hatua za kisheria wahalifu wote waliokamatwa kwa kosa hilo na kuwafikisha mahakamani.