Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali inaendelea na jitihada katika kuboresha sekta ya sheria nchini kwa kuajiri Maafisa Sheria, Mawakili wa Serikali pamoja na Mahakimu lengo likiwa ni kuhakikisha huduma bora inawafikia wananchi.

Aidha imekua ikiwawezesha watoa huduma za kisheria kwa kuanzisha Huduma za Msaada wa Kisheria, uanzishwaji wa Kamati za Ushauri wa Kisheria, Kliniki za Ushauri wa Kisheria pamoja mafunzo kwa wataalamu wa sheria na ujenzi wa maeneo ya kutolea huduma za kisheria .

Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 15, 2025 jijini Dodoma wakati alipofungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali ambapo pia amewataka Mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma na haki ili kusaidia Watanzania sambamba na kuwa washauri wazuri kwa viongozi wao.

Dkt. Biteko amesema, “Ombi langu kwenu Mawakili wa Serikali fanyeni kazi yenu kwa kuzingatia taaluma yenu ya sheria na haki, ni wajibu wenu kushauri kwa haki na fanyeni kazi bila kuogopa,fanyeni kazi ya kutetea Serikali yenu, nendeni mkaishauri Serikali na wakati wote mkatende haki, ifanyeni haki kuwa rafiki yenu, “ameeleza

Pia amewapongeza Mawakili hao wa Serikali pamoja na wadau mbalimbali kwa kuunda na kuendesha Kamati za Ushauri wa Kisheria za Mikoa na Wilaya pamoja na kuendesha Kliniki za Ushauri wa Kisheria bila malipo katika mikoa mitatu ya Dodoma, Kilimanjaro na Mwanza.

Amesema kuwa Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na Asasi za Kiraia, na binafsi katika kuwahudumia wananchi kupata huduma za kisheria. Ametaja asasi na vyama hivyo kuwa ni pamoja na Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society), Legal and Human Rights Centre (LHRC), Tanzania Legal Aid Providers (TANLAP), Legal Service Facility (LSF), Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC) pamoja na Watoa Huduma za Msaada wa kisheria kama UNDP na UN Women.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amemuelekeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushughulikia changamoto mbalimbali za Chama hicho cha Mawakili wa Serikali ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata eneo la kujenga Makao Makuu ya Chama na Vivutio vya Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali katika mikoa ya Arusha na Dodoma

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni. Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Palamagamba Kabudi amesema kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia ameimarisha sekta ya sheria kwa kutekeleza masuala mbalimbali mfano kusaidia uwepo wa haki jinai na Kampeni ya Msaada wa Sheria ya Mama Samia.

Mhe. Kabudi amesema kuwa umuhimu wa mkutano huo wa Mawakili wa Serikali kuwa ni kutoa fursa kwao ya kukutana na kujadiliana masuala ya kitaaluma, maslahi yao pamoja na kufahamiana.

Amewapongeza waasisi wa Chama hicho kwa kujenga taswira nzuri huku akiwaasa viongozi wengine watakao fuata kuendeleza taswira hiyo na amewataka mawakili hao kuwa marafiki wa Mungu badala ya Mahakama kwa kutenda haki na kusema kweli wakati wa kutimiza majukumu yao.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Hamza Johari amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kukilea chama hicho kwa miaka mitatu na kusema kuwa ni wajibu wao sasa kukilinda na kuhakikisha kinafikia malengo yake.

Pia, amebainisha kuwa kupitia mkutano huo wameidhinisha Mpango Mkakati wa Chama hicho kitakachoufuata na kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano.

“Tumetengeneza Mpango Mkakati tunaokwenda kuutekeleza kwa shauku kubwa pamoja na viongozi wapya watakao chaguliwa katika Uchaguzi unaofanyika leo,” amesema Mhe. Johari.

Amesema hadi kufikia Aprili 9, 2025 idadi ya Mawakili wa Serikali waliojisajiliwa katika Daftari la Mawakili wa Serikali imefikia 3,760 kutoka 2,652 waliosajiliwa wakati wa kuanzishwa kwa Chama hicho.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar, Mhe. Dkt. Mwinyi Talib Haji amewaomba Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia sheria ili kujenga jamii imara na kupunguza mizozo katika jamii.

Aidha, amesema taasisi za sheria ziendelee kushirikiana ili kusaidia wananchi na kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi za kuhudumia jamii na kuleta ustawi kwa mustakabali kwa maendeleo ya nchi.

Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Amedeus Shayo amesema kuwa Chama chao kimefanikiwa kujenga mfumo wa kielektoniki wa kukusanya ada kwa wanachama pamoja na kuimarisha ushirikiano na taasisi zinazoshughilika na masuala ya sheria za ndani na nje ya nchi.

“Rais Samia ameendelea kuwa kielelezo kizuri cha haki kupitia Kampeni yake ya Msaada wa Kisheria na Mawakili wanashiriki kutoa huduma za sheria kwa wananchi. Pia, agizo la Rais Samia la Mawakili kuwa walinzi wa uchumi wa nchi kwa kutumia kalamu limeweka msingi wa Chama hiki na umesaidia kuboresha sheria kadhaa mfano Sheria ya Uwekezaji,” amesema Shayo.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mstaafu na Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia kwa kuzindua Chama hicho mwaka 2022 na kusema “Chama hiki kama kilivyoanzishwa na malengo yake kitabaki kuwa Chama bora cha kitaaluma kwa sababu Serikali na mawakili walijipanga kuwa nacho na hili ni jeshi la kulinda uchumi wa nchi kwa sheria na kalamu,”