Serikali imesema itaendelea kushirikiana na kampuni za simu ili kuwasaidia wananchi katika huduma mbalimbali za kijamii zikiwamo za afya, elimu na miundombinu.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Vodacom Tanzania Foundation hivi karibuni, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kandege, amesema serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ili kuwawezesha Vodacom kuwafikia Watanzania wote wenye mahitaji.
Waziri Kandege amesema Vodacom wanafanya kazi ambazo zinagusa jamii kama masuala ya afya na kuwasaidia watoto wa kike kwenda shuleni kwa kuwapatia taulo za kike za kujihifadhi wakati wa hedhi, pia wameendelea kuwasaidia kina mama dhidi ya ugonjwa wa fistula ambao husababisha wanawake wengi kutengwa na jamii.
“Serikali itahakikisha inaimarisha miundombinu ili kuhakikisha Vodacom inawafikia watu wenye uhitaji, pia tumeona jinsi walivyoweza kuwasaidia watoto wa kike na kina mama wenye fistula juu ya kupata matibabu ya ugonjwa huo na kugawa vitaulo kwa watoto wa kike wenye uhitaji ambao wanakosa kwenda shuleni pindi wawapo kwenye hedhi,” amesema.
Amesema matarajio yake ni kuwa kazi inayofanywa na Vodacom iweze kufanywa na mashirika mengine kwa kushiriki jambo kama hilo au kwa kujiunga pamoja na Vodacom kufanya jambo hilo.
“Matarajio yangu, kazi hii inayofanywa na Vodacom isiwe yao na hayo mashirika wanayoshirikiana nayo, kwani hili ni jambo la kitaifa, hivyo ni vema mashirika mengine hata ya watu binafsi wakaendeleza juu ya hili, au wakaanzisha mambo kama haya ili kuweza kusaidia jamii zenye uhitaji kwa ujumla,” amesema.
Aidha, Mkurugenzi wa Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation na Ofisa Uhusiano, Rosalynn Mworia, amesema wamekuwa wakifanya kazi yao kwa weledi mkubwa kiasi cha kazi hizo kuibua matokeo chanya ya kazi walizokuwa wakizifanya kuanzia mwaka 2014 hadi 2017, wakiambatana na sekta binafsi pamoja na serikali kwa kuwasaidia watoto na kina mama wenye mahitaji mbalimbali.
Amesema hadi sasa wamekwisha kuwekeza Sh bilioni 11 ambazo zimewafikia kwa njia ya huduma wanawake na watoto wa kike. Amesema fedha hizo zimewafikia kupitia sekta za elimu, afya na hata uwezeshaji kiuchumi. Kwa mwaka 2019 hadi 2021, mkurugenzi huyo amesema wamejikita katika miradi ya watoto katika sekta ya elimu na utunzaji wa mazingira.
“Hadi kufikia hapa tumeshawekeza Sh bilioni 11 ambazo zimetuwezesha kuwafikia watoto wa kike na wanawake katika kuwasaidia kwenye afya pamoja na masuala ya uchumi. Kwa mwaka 2019 hadi 2021, tumejikita katika kuwasaidia watoto wa kike katika shughuli za maendeleo yanayolenga kutunza mazingira ya Tanzania,” amesema.
Pia amesema watajikita zaidi katika maeneo ya elimu na kiuchumi kwa ujumla ili kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kujikwamua.
“Tutajikita katika maeneo ya elimu na uchumi kwa ujumla ili kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kwa ujumla kujikwamua kutoka pale walipo ili kuweza kusaidia taifa kufikia uchumi wa kati mwaka 2025,” amesema.