Kama tujuavyo nchini Tanzania kuna shule za aina mbili: Shule za Serikali (ambazo pia huitwa shule za umma) na shule za watu binafsi.
Katika Tanzania ya leo, shule za Serikali ni nyingi zaidi kuliko shule za watu binafsi. Hali haikuwa hivyo wakati wa ukoloni na katika miaka ya mwanzo ya Uhuru. Wakati huo shule za watu binafsi zilikuwa nyingi zaidi kuliko za Serikali.
Sehemu kubwa ya shule za watu binafsi wakati huo ilikuwa shule za misheni. Shule za Serikali au za umma zilikuwa chache sana.
Pengine hapa si vibaya nikitoa mfano hai kutoka wilaya yangu ya Masasi. Mpaka mwaka 1969 Serikali ilipotaifisha shule za watu binafsi, Masasi ilikuwa na shule za msingi 138. Kati ya hizo, shule 136 zilikuwa za misheni na mbili zilikuwa za Serikali, tena Halmashauri ya Wilaya. Serikali Kuu haikuwa na shule hata moja.
Shule za misheni zilitoa mchango mkubwa sana katika maendeleo ya elimu Tanganyika. Watumishi wengi wa Serikali walikuwa walipata elimu katika shule za misheni.
Wakati ule Gavana wa Pili wa Tanganyika, Donald Cameron, alitambua mchango mkubwa wa misheni katika sekta ya elimu. Kwa hiyo, kuanzia mwaka 1927 Serikali yake ilianza kutoa ruzuku (misaada ya fedha) kwa shule za misheni.
Ukitaka kusema kweli, hata katika Tanzania yetu ya leo, viongozi wengi wa Serikali — Waislamu kwa Wakristo — wamepitia shule za misheni.
Mwaka 1969 Serikali chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere ilitaifisha shule za watu binafsi ambazo karibu zote zilikuwa za misheni. Hii ilitoa nafasi kwa mtoto wa Tanzania katika kusoma shule yoyote.
Kuanzia wakati huo shule za Serikali ni nyingi zaidi kuliko shule za watu binafsi. Hata hivyo, katika maendeleo ya elimu, shule za watu binafsi zinafanya vizuri zaidi. Na zipo sababu.
Shule za watu binafsi zinajitosheleza kwa vifaa vya kufundishia. Tena walimu wa shule za watu binafsi wanafanya kazi kwa furaha. Mishahara yao inaridhisha. Hii inawapa ari ya kufundisha. Kwa hiyo, shule hizo zina matokeo mazuri ya mitihani.
Leo viongozi wengi wa Serikali — wabunge na watu wenye uwezo mzuri wa kiuchumi — hupeleka watoto wao katika shule za msingi za watu binafsi. Shule za Serikali zimebaki kuwa shule za watu maskini Tanzania. Mtu mwenye uwezo mzuri kifedha hawezi kumpeleka mtoto wake katika shule hizi.
Kwa jumla, katika hali halisi, na ukitaka kusema kweli, Serikali haitofautiani na baba ambaye hajali watoto wake! Serikali inaona na inatambua kuwa shule zake mambo yake ni ovyo ovyo, lakini haichukui hatua kurekebisha hali ya mambo. Badala yake inashindanisha shule zake na shule za watu binafsi. Katika hili Serikali haitendi haki kwa shule zake.
Kwa upande mmoja, shule za Serikali hazina vifaa vya kutosha, na imeshikilia kusambaza vitabu visivyokidhi mahitaji katika shule zake, pengine ni kwa sababu watoto wa wakubwa hawasomi kwenye shule hizo. Kwa hiyo, si kitu kwa Serikali watoto wa maskini wakipewa elimu mbovu!
Katika hali hiyo, watoto wa wakubwa wataendelea kurithishana madaraka serikalini, na hata bungeni kwa kuwa wao ndiyo wanaopata elimu nzuri na ya juu. Watoto wa maskini wataendelea kutawaliwa tu kwa muda usiojulikana.
Katika Tanzania ya leo, elimu inatolewa kibaguzi kama ilivyokuwa wakati wa mkoloni. Inashangaza kuona kwamba hata fedha ya chenji ya rada iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya kununua madawati ya shule za Serikali za watoto wa maskini ‘imeyeyuka’. Watoto wengi wa maskini wanaketi sakafuni au wanabanana kwenye madawati. Serikali haitendi haki kwa shule zake!
Na kwa upande wa walimu wa shule za Serikali hali ni mbaya. Mishahara yao ni midogo. Kwa hiyo, wengi huishi kwa kukopa au kwa fedha za tuition. Imefika mahali ambapo baadhi ya walimu hawaendi shuleni ili kukwepa madeni.
Cha kushangaza ni kuona kwamba Serikali haichelewi kuwaongezea wabunge posho zao. Leo mbunge anapata posho ya Sh 300,000 kwa siku wakati mwalimu wa kawaida katika shule ya Serikali hapati mshahara wa Sh 300,000 kwa mwezi baada ya kukatwakatwa mshahara wake! Serikali haitendi haki kwa shule zake. Na hali hii inachochea walimu kuichukia Serikali chini ya chama tawala — Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kibaya zaidi, katika mazingira hayo yote, Serikali inashindanisha shule zake na shule za watu binafsi!
Kwa hiyo, unakuta kwamba katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba, nafasi 10 bora hushikwa na shule za watu binafsi. Kwa bahati mbaya Serikali haijatambua hali hii inavyoidhalilisha Serikali yenyewe, lakini pia inawakatisha tamaa na kuwadhalilisha walimu wa shule za Serikali kwamba hawafundishi vizuri.
Tunajua mara nyingi Serikali haisikii kitu. Inaamini haikosei. Lakini ni vyema Serikali ikatenganisha matokeo ya mitihani ya shule za Serikali na ya shule za watu binafsi ili kupata ushindani wa haki kila upande.
Kwa bahati mbaya pia wanafunzi wengi wa darasa la saba wa shule za watu binafsi wanaofaulu Mtihani wa Taifa hawaendi kusoma kwenye shule za sekondari za watu binafsi. Wanakwenda kujiunga na shule za sekondari za Serikali. Kwa kuwa ni wao wanaofanya vizuri sana katika Mtihani wa Taifa, basi ni wao wanaojaza nafasi za masomo kwenye shule bora za Serikali.
Watoto wa maskini huishia kwenye shule za sekondari za kata. Huo ni mwendelezo wa Serikali wa kutozitendea haki shule zake za msingi na watoto wa maskini wanaosoma katika shule hizo!
Umefika wakati Serikali ijitafakari upya, ibadilike sasa kwa kuanza kuzitendea haki shule zake na watoto wa maskini. Elimu bora itolewe kwa watoto wote wa Tanzania kwa usawa.