Vyombo vya habari nchini vinafanya kazi ya kuibua uozo. Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli kuwa kila vinapogusa vyombo vya habari inafuatilia na kubaini kuwa kuna uozo. Vyombo vya habari kwa muda mrefu vimekuwa mstari wa mbeli kuibua uozo serikalini. Hata hivyo, ni bahati mbaya havikusikilizwa.
Ni bahati mbaya kuwa Serikali ya Awamu ya Nne haikupata kuamini vyombo vya habari kama chanzo muhimu cha taarifa kwa ajili ya maendeleo ya jamii kama zifanyavyo nchi zilizoendelea.
Serikali ya Awamu ya Tano, imerejesha uhai kwa vyombo vya habari. Kila kinachotamkwa kwenye vyombo vya habari sasa kinachunguzwa, kinafuatiliwa na kutolewa jibu.
Sisi tunafurahi kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Maguguli wamekuwa mstari wa mbele kufuatilia maovu yanayochapishwa na vyombo vya habari kisha kuchukulia hatua wahusika kupitia dhana ya ‘kutumbua majipu.’
Sisi gazeti la JAMHURI, tumefarijika si kwa sababu Rais Magufuli ametutaja waziwazi na kutusifia kwa kufanya kazi iliyotukuka ya uchunguzi wenye kuanika ukweli katika masuala mbalimbali, bali kwa mwelekeo wa serikali yake ya kuheshimu na kuthamini kazi inayofanywa na vyombo vya habari.
Rais Magufuli amekaririwa akisema kuwa wapo watu wanaobeza kazi yake ya kufuatilia anayobaini yeye au kupitia vyombo vya habari kuwa kuna uozo kisha akachukua hatua kama alivyofanya katika suala la mita za kupima mafuta yanayoingia nchini, ila akawaonya.
Katika onyo, lake Februari 13, mwaka huu, alisema kama wapo watu wanadhani kuwa hatua anazochukua ni nguvu ya soda, wajue wamepotoka. Kwa maneno yake alisema kuwa: “Soda ikichanganywa na gongo utalewa tu.” Maneno haya yanajinasibu na jina lake la Pombe, ila ni wazi alimaanisha jambo.
Serikali yake tayari imeweza kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 1.8 kwa mwezi kiasi ambacho ni mara mbili ya kiwango klichokuwa kinakusanywa na Serikali iliyomtangulia. Hapa tunachosema sisi ni kuwa kasi ya makusanyo iendelee, na mipango ya uwekezaji isimamiwe na waziri mwenye dhamani kwa ajili ya ukusanyaji endelevu
Ni ukweli usiopingika milele kuwa makusanyo tunayoyashuhudia leo yanatokana na dhana ya ukweli na uwazi. Kwamba wanaodaiwa wanalipa na kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha inawawezesha wanaolipa waendelee kulipa sasa na baadaye.
Sisi tunasema yote hayo yatawezekana kwa kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari ambavyo mara zote vinafanya kazi ya kuonyesha panya amekimbilia wapi kisha vyombo vyenye dhamana vikafanya kazi ya kukamata panya aliyetajwa.
Kwa vyovyote iwavyo, Serikali ikiviwezesha vyombo vya habari kufanya kazi yake kwa uhuru unaostahili, basi iwe isiwe, vitasaidia jamii ya Watanzania kukusanya kodi kubwa na hivyo kuwezesha huduma za jamii kuimarika.
Ni kwa njia hii tunaomba Serikali iwezeshe kutunga sheria inayoviwezesha vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru.