Mhariri,

Ninaona fahari kutumia nafasi hii katika Gazeti Jamhuri kuifikishia Serikali kilio cha wananchi katika kata ya Komuge, Wilaya ya Rorya mkoani Mara, ambao kwa muda mrefu sasa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji.

Tumekuwa tukitoa kilio hiki kwa viongozi wetu akiwamo Mbunge wa Jimbo la Rorya, Lameck Airo, lakini hakuna dalili zozote za kushughulikia kero hii ili wananchi wa kata hii waweze kupata maji ya kutosha, huduma ambayo kimsingi ndiyo inawezesha kwa asilimia kubwa uhai wa binadamu, wanyama na mimea.

Tatizo la uhaba wa maji katika kijiji cha Irienyi na kata ya Komuge kwa ujumla linakwaza shughuli za uzalishaji mali na maisha ya wakazi wa eneo hili.

Kwa mfano, ukitembelea shule mbalimbali za msingi na sekondari katika kata ya Komuge utashangaa kuona sare za wanafunzi wengi zimechafuka kwa kiasi cha kutisha kutokana na kukosa maji ya kuzifua.

Lakini pia, tatizo la uhaba wa maji linasababisha wanawake wengi kutolala usingizi usiku, badala yake wanatumia muda mwingi kutembea umbali mrefu kwenda kupanga foleni za kuchota maji katika visima vichache vilivyopa, wakati mwingine kuanzia saa tisa usiku hadi saa sita mchana.

Ikumbukwe kuwa tatizo la uhaba wa maji linaikabili kata ya Komuge licha ya uwepo wa Ziwa Victoria ambalo halipo umbali mrefu sana kutoka katani hapa.

Kupitia gaziti hili makini, ninaiomba Serikali kupitia kwa Waziri wa Maji, Profesa  Jumanne Maghembe, isikie kilio chetu na hivyo, ichukue hatua ya kututatulia kero ya uhaba wa maji katika kata ya Komuge ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na ujenzi wa taifa letu.

Pia kijiji cha Irienyi kinakabiliwa na ukosefu wa huduma ya umeme. Tunaiomba pia Serikali ishughulikie tatizo hili kwa kutuletea mtandao wa nishati hiyo katika kijiji hiki ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi miongoni mwa wananchi kijijini hapa.

Chacha Mgaya, Komuge – Rorya

0786 640 150