Na Deodatus Balile, Mtwara
Leo naandika makala hii nikiwa mjini
Mtwara. Nimefika Mtwara Ijumaa asubuhi.
Ni mwaka wa tatu sasa tangu nimetoka
Mtwara. Naikumbuka Mtwara ya mwaka
2015, taarifa za ugunduzi wa gesi
zilipoenea kila kona. Nakumbuka magari
makubwa niliyokuwa nakutana nayo katikati
ya mji wa Mtwara na ghafla mji
ulivyobadilika ukawa kama Dar es Salaam
enzi hizo.
Nimepita katika nyumba za National
Housing (NHC) zilizopo katikati ya Mji wa
Mtwara, ambazo sehemu ya nyumba hizo
zimepangishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT). Nyingine hazina wapangaji.
Nimesikiliza mnyukano uliotokea bungeni
kati ya wabunge na serikali wakibishania
hatua ya Serikali Kuu kuchukua asilimia 65
ya ushuru wa mauzo ya korosho.
Kiasi kinachogombewa na kupasua nchi
kisiasa ni Sh. bilioni 201. Wala hapa sihitaji
kumwita mzee Andrew Chenge au
kumwomba kuazima maneno yake kuwa
“hivi ni vijisenti”
, kwa nini viligawe taifa?
Nafahamu katika hali ya umaskini
tuliyonayo, kiasi hiki cha fedha kikiingia
katika mkoa mmoja au mitatu, kila kona
itachemka.
Sitanii, mjadala uliojitokeza umenipa somo.
Umenifanya niwaze, tunawezaje
kujikomboa kama nchi tukazalisha matajiri
wapya wakalipa kodi kuliko kuvizia ushuru
wa mauzo ya korosho? Nimejaribu
kuangalia utajiri wa watu watano tu duniani.
Tajiri namba moja ni Jeff Bezos, ambaye
kwa mujibu wa jarida la Forbes, kwa sasa
utajiri wake ni dola bilioni 112 au Sh. trilioni
252 za Tanzania. Hizi trilioni zinaandikwa
hivi; 252,000,000,000,000. Kwa mwaka jana
pekee, amepata faida ya dola bilioni 39 au
Sh. trilioni 87.75. Unaweza kuziandika hivi;
87,750,000,000,000. Huyu ni mmiliki wa
kampuni ya biashara ya mtandaoni ya
Amazon. Hapa kwetu Tanzania soko la
mtandaoni tunalichezea.
Bajeti ya Tanzania ambayo imejadiliwa kwa
miezi miwili jijini Dodoma ni sawa na dola
bilioni 14.2 au Sh. trilioni 32. Ukipenda
unaweza kuiandika hivi; Sh.
32,000,000,000,000. Bila kufanya biashara
yoyote, Jeff Bezos akiamua kuitunza
Tanzania kwa fedha alizonazo sasa
anaweza kulipa bajeti yote ya mwaka kwa
muda wa miaka 7 na miezi 8. Kila kitu
kilichopangwa kwenye bajeti kitapatikana
bila nchi yetu kukusanya kodi hata senti
tano au mtu yeyote kufanya kazi.
Tajiri wa pili duniani, Bill Gates, utajiri wake
katika mwaka 2018 ni dola bilioni 90 au Sh.
trilioni 202.5 kwa kubadilisha dola moja kwa
Sh. 2,250. Kwa kiwango cha bajeti yetu ya
Sh. trilioni 32, Bill Gates ana uwezo wa
kulipa bajeti ya taifa la Tanzania kwa miaka
6.3. Tajiri wa tatu ni Warren Buffett,
mwenye utajiri wa dola bilioni 84, sawa na
Sh. trilioni 189. Hizi nazo zinaandikwa hivi;
189,000,000,000,000.
Tajiri wa nne ni Bernard Arnault na familia
yake, wakiwa na utajiri wa dola bilioni 72,
sawa na Sh. trilioni 162. Hizi nazo unaweza
kuziandika hivi; 162,000,000,000,000. Tajiri
wa tano duniani ni Mark Zuckerberg
mwenye dola bilioni 71, sawa na Sh. trilioni
159.75. Ukipenda unaweza kuziandika hivi
159,750,000,000,000. Huyu ni mmiliki wa
Facebook, WhatsApp na mitandao mingine
kadhaa ya kijamii ambayo hapa kwetu
tunaifunga. Zuckerberg amezaliwa Mei 14,
1984.
Sitanii, miongoni mwa matajiri hawa watano
wakubwa, wanne ni Wamarekani. Bernard
Arnault pekee ndiye Mfaransa. Dunia hii ina
matajiri wenye angalau dola bilioni 5 kila
mmoja wapatao 2,200. Usiniulize Tanzania
wako wangapi wenye utajiri wa kiwango
hiki.
Matajiri hawa wanalipa serikalini wastani wa
dola bilioni 2 hadi 5 kwa mwaka kwa njia ya
kodi mbalimbali kila mmoja. Kampuni ya
ndege kama Boeing, ambako tunanunua
ndege ya Boeing 787-800, kwa mwaka jana
tu, imelipa kodi ya makampuni kwa Serikali
ya Marekani ipatayo dola bilioni 1.2.
Ukichanganya kodi zote inazolipa kupitia
huduma, bidhaa, VAT na PAYE, zinafikia
karibu dola bilioni 10. Bajeti ya taifa letu ni
dola bilioni 14.2.
Tunahitaji kuwa na matajiri wawili wa aina
ya Mark Zuckerberg wakalipa kodi zenye
uwezekano wa kuendesha bajeti ya taifa
letu. Ni kwa msingi huo, napenda kuchukua
fursa hii kuishauri serikali ianzishe mpango
maalumu wa kuwezesha wazawa na
hatimaye kuzalisha matajiri wazalendo
watakaokuwa na uwezo wa kulipa kodi,
tukaacha kukimbizana na wakulima wa
korosho.
Tusipofanya hivyo na tukakosa mahala pa
kupata kodi, tutafirikia kurejesha kodi ya
kichwa si muda mrefu. Mungu apishe mbali.
Wiki ijayo nitaeleza hatua walizochukua
Morocco na Ethiopia kujenga matajiri kwa
njia ya viwanda na uwekezaji kati ya mwaka
2010 na sasa.
Mwisho