*Asisitiza kuwa mifugo ni uchumi, ajira na biashara
*Atoa wito kwa wakulima na wafugaji wawe wamoja
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha sekta ya mifugo inakuwa endelevu na yenye tija.
Amesema kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mara zote ameweka msisitizo katika kuiendeleza sekta hiyo kwa kuwa mifugo ni uchumi, ajira na ni biashara.
Ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipozungumza na wananchi katika mikutano aliyoifanya jana Jumatano (Machi 12, 2025) Wilayani Igunga, mkoani Tabora ambapo yupo kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili.
“Tunawahamasisha wafugaji, fugeni mifugo ni uchumi, mifugo ni maisha na mifugo ni pesa na wakulima limeni tupate mazao mengi ya chakula na biashara na ni lazima wafugaji na wakulima tuelewane.”

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini kuweka mikakati ya kuhakikisha wanakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kuzisimamia fursa zilipo kwenye maeneo yao ili kuwanufaisha wananchi. “Mkifanya hivyo mtakuwa mmewasaidia wananchi kujiendeleza kiuchumi.”
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye shule ya Sekondari ya Seif Gulamali, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka jamii kuweka nguvu za pamoja katika kumlinda mtoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikakati iliyopo katika sekta ya elimu ili sekta hiyo iweze kuwanufaisha watanzania kwa kukuza ubora wa elimu nchini.


