WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya tano itaendelea kusimamia maadili ya utumishi wa umma ili kuenzi fikra za hayati Edward Moringe Sokoine.
“Tutaendelea kusimamia maadili ya utumishi wa umma kwa kuzingatia yale yote ambayo Mheshimiwa Sokoine aliyaanzisha,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Aprili 12, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi waliohudhuria ibada ya kumbukumbu ya miaka 34 ya kifo cha Sokoine, iliyofanyika kijijini kwake Engwiki, kata ya Monduli Juu, wilayani Monduli, mkoani Arusha.
Ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Mhashamu Josephat Lebulu, ilihudhuriwa na viongozi wa dini wa wilaya, viongozi wa Serikali na wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Tate ole Nasha na baadhi ya wabunge.
Waziri Mkuu amesema Mhe. Sokoine alikuwa adui wa wahujumu uchumi na alihakikisha uchumi wa nchi unakua kwa maslahi ya Watanzania wote. “Mungu alitupa hazina iliyong’ara na kuangaza. Sote tuendelee kuangaza kwa kutenda mema na kuendeleza yale yote aliyoyaanzisha mpendwa wetu,” alisema.
“Katika maisha yake, hakuwa na ubinafsi, uroho, wala tamaa ya kujilimbikizia mali. Hili ni jambo la kuigwa na sisi viongozi wa umma. Nasi tulioko kwenye nafasi hizi za uongozi, tumuombe Mungu atuwezeshe tutende yale aliyoyaanzisha,” alisisitiza.
Alitumia fursa hiyo kuwafikishia wanafamilia na wananchi waliohudhuria ibada hiyo, salaam za pole kutoka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan.
Mapema, akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria ibada hiyo, Askofu Mst. Lebulu alimuelezea hayati Sokoine kuwa ni kiongozi aliyechapa kazi kwa bidii, mwenye uzalendo, aliyeongozwa na upendo na uwajibikaji kwa wananchi anaowaongoza.
“Ili tuweze kuwajibika na kuwa wazalendo kwelikweli, tunapaswa kuwa waaminifu na watu tunaomcha Mungu. Mtu awaye wa dini yoyote ile, kama hamchi Mungu, hawezi kuwa muwajibikaji.”
Alisema kila mtu anapaswa kumheshimu mwenzake kwa dini na imani yake. “Tuheshimiane kila mmoja kwa dini na imani yake, kwa sababu sote tumeumbwa kwa sura na mfano wake. Siyo kwamba tuvumiliane, tunatakiwa tusidharauliane bali tuheshimiane,” alisisitiza.
“Ni lazima tuwe waaminifu, tuache unafiki, tuache kuwa na maisha yenye hila na hiyana na badala yake, tuongozwe na dhamiri safi. Tuwe waaminifu kwa wenzetu, kwa dini na imani zetu na zaidi ya yote tuwe waaminifu kwa nchi yetu,” alisema.
“Ni aibu kukuta Mtanzania anaitukana nchi yake. Tupende vijiji vyetu, tarafa zetu, mikoa yetu na nchi yetu. Tuipende, tuitunze na tuilinde ili iwe nchi bora. Tuwe mfano kwa watoto wetu na wazazi wetu katika kuijali nchi yetu,” alisisitiza.
Naye, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Kabudi alipopewa nafasi awasalimie wananchi, alisema kuna watu wanakufa lakini bado wanaendelea kuwa hai na kwa hilo, wanafamilia wanapaswa kuendelea kumshukuru Mungu.
“Tangu alipofariki mwaka 1984, hakuna mtu aliyejua kwamba hadi sasa, ambapo ni miaka 34 imepita, Edward Moringe Sokoine ataendelea kuwa hai. Ninasema yu hai kwa sababu maneno na matendo yake, bado yanaishi,” alisema.
“Edward Moringe Sokoine amegoma kufa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere amekataa kufa. Na sisi wasaidizi wa Rais Magufuli, tunapaswa kujitoa kwa wananchi na Taifa; kujiongeza zaidi katika utumishi wetu na hasa kuwajibika kwa kulitumikia zaidi Taifa kuliko kudai mapato ili tutakapoitwa kwenye promosheni iliyo kuu, wanaosalia waone faida ya kuwepo kwetu hapa duniani,” alisema huku akishangiliwa.
Akitoa shukrani kwa niaba ya familia, msemaji wa familia ya marehemu Sokoine, Bw, Lembris Kivuyo alisema wanaishukuru Serikali kwa jinsi ambavyo imekuwa karibu sana na familia hiyo tangu Mhe. Sokoine alipofariki.
“Tunaishukuru sana Serikali na tunazidi kuwasihi Watanzania waendelee kumuombea Mheshimiwa Rais Magufuli ili aendelee kuongoza Taifa hili bila ajizi na sisi kama familia tutaendelea kumuunga mkono Mhe. Rais katika jitihada zake za kutetea rasilmali za Taifa,” alisema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, APRILI 12, 2018.